Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Shilla; Kutoka Azam FC hadi mitaa ya Ibrahimovic

SHILLA Pict

Muktasari:

  • Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 18 anakipiga katika Klabu ya AIK inayoshiriki Ligi Kuu Sweden maarufu kama Allsvenskan   aliyojiunga nayo msimu uliopita akitokea Azam FC ambako alipata nafasi hiyo baada ya kufaulu majaribio.

KUTOKA viwanja vya Azam Complex hadi kwenye ardhi ya Sweden ambako mastaa kama Zlatan Ibrahimovic waliwahi kuandika historia kubwa kwenye soka la Ulaya, Mohamed Shilla sasa anapambana kuandika historia yake mwenyewe.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 18 anakipiga katika Klabu ya AIK inayoshiriki Ligi Kuu Sweden maarufu kama Allsvenskan   aliyojiunga nayo msimu uliopita akitokea Azam FC ambako alipata nafasi hiyo baada ya kufaulu majaribio.

Shilla alijiunga na chama hilo baada ya kumalizika kwa msimu wa 2025/26 akiwa mchezaji bora wa ligi ya vijana ambapo Azam FC ilikuwa bingwa wa mashindano hayo.

Katika mahojiano na Mwanaspoti, Shilla amezungumzia mambo mbalimbali yanayohusu maisha yake ya soka barani Ulaya, uzoefu anaoupata ugenini, pamoja na mchango mkubwa wa mfumo wa malezi wa Azam FC uliomjenga hadi kufikia hapo alipo.


SHI 05

MABAO 12

Msimu uliopita, kijana huyo alionyesha ubora wa hali ya juu kwa kufunga mabao 12 na kutoa pasi saba za mabao , takwimu ambazo kwa mchezaji anayetoka Afrika na kuingia kwenye mfumo wa soka la Ulaya ni za kujivunia.

Akizungumzia mafanikio hayo, Shilla anasema: “Kwanza kabisa ni kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa sababu kuanza vizuri kunakupa mwanzo mzuri wa kuweza kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Unapotoka chini unaenda juu ambapo ndipo unakutana na upinzani unaokufanya ukue.”

Shilla anafafanua kuwa upinzani anaokutana nawo ligi ya Sweden umemsaidia kujitambua na kujua uwezo wake halisi, jambo linalomfanya acheze kwa viwango vya juu kila anapopewa nafasi.

Anaongeza kuwa kiwango hicho kimempa motisha kubwa na anaamini msimu huu utakuwa bora kwake na atavunja rekodi ya msimu uliopita.

“Sio rahisi lakini naamini rekodi hiyo ya mabao nitaivunja unajua ni ngumu ila mimi huwa napenda kujitathmini mimi mwenyewe na kujiwekea malengo.”


SHI 04

BARIDI CHANGAMOTO

Kiungo huyo anasema moja ya changamoto kubwa nchini humo ni baridi zaidi na baadhi ya vyakula ambavyo hajazoea kula lakini anajitahidi kuendana navyo.

“Huku baridi sana tofauti na nyumbani hapa joto ni kali ila inakuwa baadhi ya kipindi tu, nafikiri hilo ndio changamoto kubwa tu kwangu na chakula basi,” anasema.


SHI 03

VITA NA SABRI KONDO

Ligi ya Sweden imekuwa miongoni mwa ligi zinazowapa fursa vijana wengi wa Kitanzania. Mbali na Shilla, yupo pia Mtanzania mwenzake, Sabri Kondo, anayekipiga BK Hacken ya Sweden.

Mwanaspoti lilipotaka kujua kama nyota hao huwa wanakutana na kusaidiana, Shilla anaeleza kuwa ingawa wamo kwenye nchi moja, ushindani wa uwanjani na umbali wa miji unawafanya wakutane zaidi wakati wa michezo yao.

“Tumeshakutana katika michezo miwili, na hiyo mechi haiwezi ikawa rahisi hata siku moja. Lazima iwe mechi ngumu kwa sababu kila mmoja anataka kuipigania timu yake,” anasema mchezaji huyo huku akitabasamu.

Kuhusu maisha ya nje ya uwanja na kutembeleana, Shilla anasema: “Tunapokaa mimi na anapokaa Sabri ni miji tofauti kabisa, kwa hiyo inakuwa ngumu kutembeleana mara kwa mara. Lakini tunapokutana kwenye michezo au mikusanyiko ndipo tunapopata muda wa kupiga stori, na pia huwa tunawasiliana sana kwa njia ya simu.”


SHI 02

AZAM FC MKOMBOZI WA VIJANA

Moja ya vitu vinavyowasumbua wachezaji wengi wa Kitanzania wanapokwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi ni mabadiliko ya mfumo wa maisha. Hata hivyo, kwa Shilla hali ilikuwa tofauti kutokana na msingi mzuri alioupatia Azam FC.

“Azam ni kituo ambacho naweza kusema ni bora sana kwa Ukanda wa Afrika Mashariki. Kinatengeneza na kinazalisha wachezaji kwa asilimia kubwa hapa nchini, na wengi wanaokwenda nje lazima wawe wamepita kwenye akademi yao,” anasema Shilla na kuongeza: “Azam haikufundishi tu mpira wa uwanjani, bali inakufundisha pia jinsi ya kuishi ukiwa kambini na hata ukiwa nje ya kambi. Maisha ya kule yanakurahisishia hata unapoenda nje ya nchi, haujisikii kama ni mgeni au mpweke sana kwa sababu tayari ulishazoea mazingira ya kuishi.”


SHI 01

SAMATTA WA BAADAYE

Kocha wa zamani wa vijana wa Azam FC, Mohamed Badru, aliwahi kunukuliwa akisema kuwa Mohamed Shilla na Cyprian Kachwele ni miongoni mwa wachezaji watakaokuja kuwa Mbwana Samatta wa baadaye  kwenye soka la Tanzania.

Mwanaspoti ilipomuuliza kuhusu kauli hiyo ya mwalimu wake wa zamani, Shilla alisema: “Mwalimu Badru ni kocha aliyetufundisha kwa muda mrefu na ndiye aliyetuchagua kujiunga na Azam. Ni hatua kubwa sana kufananishwa na mtu kama Samatta kwa sababu kila mchezaji kijana anatamani kucheza Ulaya na kufanikiwa ili kuitangaza nchi yake.”

Shilla anahitimisha kwa kusema kuwa anaamini kupitia nidhamu, bidii na kujituma uwanjani, malengo yake na ya vijana wengine wanaopambana nje ya nchi yatafikiwa.

“Kila kitu kinawezekana ukiweka bidii na nidhamu. Lengo letu ni kuendelea kupeperusha bendera ya Tanzania na kufungua milango kwa vijana wengine wanaokuja nyuma yetu,” anasema mchezaji huyo.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 18 anasema anaamini wana nafasi ya kufanya vizuri kwenye mashindano ya kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 23 dhidi ya Kenya.

“Kupata nafasi kwanza ya kuitwa tu ni heshima kwangu kwa sababu ni mara yangu ya kwanza na mimi pamoja na vijana wenzangu tuna matarajio makubwa ya kufanya vizuri.”