Shadrack Nsajigwa ala kiapo Tanzania Prisons
Muktasari:
- Baada ya hapo, timu hiyo ikacheza Play-Off nyingine ya kujinasua na janga la kushuka daraja dhidi ya Polisi Tanzania iliyoitoa Mbeya Kwanza kwa jumla ya mabao 7-1, kisha safari ya Prisons ikaishia hapo kwa kuchapwa jumla ya mabao 4-1.
KOCHA Mkuu wa Tanzania Prisons, Shadrack Nsajigwa 'Fuso', amesema licha ya ushindani mkubwa msimu huu, ila atahakikisha anarejesha heshima ya kikosi hicho chenye maskani yake jijini, Mbeya, ili kirejee tena Ligi Kuu Bara msimu wa 2027-2028.
Akizungumza na Mwanaspoti, Nsajigwa amesema ili kurejesha matumaini ya mashabiki wa timu hiyo ni kuhakikisha wanapata matokeo mazuri uwanjani, jambo litakalochangia kupata sapoti kubwa kutoka kwao, hasa wanapocheza mechi zao za nyumbani.
"Unaposhinda hata hali ya kujiamini kwa wachezaji inakuwa ni kubwa, tumeanza mechi mbili ugenini na kupata pointi tatu kati ya sita tulizopaswa kuzipata, hii inaonyesha ushindani ni mkubwa na tunapaswa kujipanga zaidi," amesema Nsajigwa.
Nsajigwa aliyeanza msimu wa 2025-2026, akitokea Transit Camp, alijiunga na Prisons, Februari 27, 2026, akichukua nafasi ya Mkenya Zedekiah 'Zico' Otieno, aliyeondoka kikosini humo cha maafande Februari 25, 2026, kutokana na matokeo mabaya.
Kocha huyo aliyeichezea Prisons, Yanga na timu ya taifa ya Taifa Stars, kwa msimu wa 2025-2026, alikiongoza kikosi hicho cha maafande kumaliza nafasi ya 13 na pointi 32, katika Ligi Kuu Bara, jambo lililochangia kiasi kikubwa kushuka daraja. Maafande wa Tanzania Prisons walishuka daraja kupitia Play-Off, baada ya kumaliza nafasi ya 13 na pointi zao 32, huku ikicheza na kikosi cha Mbeya City kilichomaliza kikishika nafasi ya 14 na pointi 30 na kutolewa kwa jumla ya mabao 2-0.
Baada ya hapo, timu hiyo ikacheza Play-Off nyingine ya kujinasua na janga la kushuka daraja dhidi ya Polisi Tanzania iliyoitoa Mbeya Kwanza kwa jumla ya mabao 7-1, kisha safari ya Prisons ikaishia hapo kwa kuchapwa jumla ya mabao 4-1.