Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Championship 2026/27 vita bado ni mbichi

CHAMPIONSHIP Pict

Muktasari:

  • Mechi zilizopigwa jana Ijumaa, zilishuhudiwa TMA FC ikiikaribisha Stand United maarufu ‘Chama la Wana’, kwenye Uwanja wa Sokoine jijini, Mbeya, huku Gunners FC ikicheza dhidi ya kikosi cha Kigamboni United, kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

UHONDO wa Ligi ya Championship umeingia raundi ya tatu jana na kushuhudia ushindani ukiendelea kuonekana mapema kwa timu shiriki, huku mechi nyingine zikipigwa leo Jumamosi na nyingine kuchezwa pia kesho Jumapili kwenye viwanja mbalimbali.

Mechi zilizopigwa jana Ijumaa, zilishuhudiwa TMA FC ikiikaribisha Stand United maarufu ‘Chama la Wana’, kwenye Uwanja wa Sokoine jijini, Mbeya, huku Gunners FC ikicheza dhidi ya kikosi cha Kigamboni United, kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Mechi nyingine tatu zinapigwa leo Jumamosi, ambapo Songea United iliyotoka suluhu (0-0), dhidi ya Rhino Rangers, itakuwa kwenye Uwanja wa Majimaji, uliopo mjini Songea mkoani Ruvuma kucheza dhidi ya kikosi cha IAA SC kutoka jijini, Arusha.

IAA SC ambao ni wageni wapya katika Ligi ya Championship inayoshiriki msimu wa 2026-2027, kwa mara ya kwanza, ina kazi nyingine kubwa ya kutafuta ushindi, baada ya mechi iliyopita kikosi hicho kuchapwa mabao 2-0, na KenGold ya Mbeya.

MASTA 03

Timu ya IAA SC ya Arusha ilifuzu kucheza Ligi ya Championship kwa msimu wa 2026-2027, kupitia mechi ya ‘Play-Off’, baada ya kuitoa African Sports ya Tanga kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda nyumbani 2-1, kisha ugenini ikatoka sare ya bao 1-1. Kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini, Tanga, wenyeji Bigman FC iliyochapwa mechi zote mbili mfululizo, inapambana kutafuta ushindi wa kwanza msimu huu, wakati kikosi hicho kitakapopambana na maafande wa Transit Camp iliyoichapa TMA FC bao 1-0.

Bigman FC iliyohamishia makazi yake Tanga baada ya msimu wa 2025-2026, kuweka kambi Lindi, ilianza msimu wa 2026-2027, kwa kuchapwa mabao 2-1, dhidi ya IAA SC ya Arusha, kisha wiki iliyopita ikachapwa tena na KMC FC ya Dar es Salaam 3-1.

Mbeya Kwanza iliyoanza msimu kwa kusuasua na kuchapwa mechi zote mbili za mwanzoni, itakuwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini, Tabora kucheza na Bandari Tanzania yenye kumbukumbu nzuri baada ya kuichapa Gunners FC ya Dodoma bao 1-0.

MASTA 07

Kikosi hicho cha Mbeya Kwanza kilichoshuka daraja msimu wa 2021-2022, kimechapwa mechi mbili za mwanzo, ikianza na mabao 2-1, dhidi ya Stand United ‘Chama la Wana’, kisha ikachapwa 2-1, wiki iliyopita kutoka kwa maafande wa Tanzania Prisons.

Kwa upande wa Bandari Tanzania inayoshiriki Ligi ya Championship kwa mara ya kwanza, mechi ya leo ni ya tatu kucheza ugenini, baada ya sare ya bao 1-1, dhidi ya KenGold FC ya jijini, Mbeya, kisha kuichapa Gunners FC ya Dodoma bao 1-0.

Bandari ilimaliza vinara kundi A na pointi 32, katika Ligi Daraja la Kwanza msimu wa 2025-2026, baada ya kushinda mechi 10, sare mbili na kupoteza mbili kati ya 14, iliyocheza huku ikifunga mabao 25 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa tisa.

Ligi hiyo itaendelea tena kesho Jumapili kwa mechi tatu kupigwa, ambapo KMC FC iliyoichapa Bigman FC ya Tanga mabao 3-1, itakuwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge jijini, Dar es Salaam, kucheza dhidi ya KenGold FC iliyoifunga IAA SC 2-0.

MASTA 08

KMC FC iliyoshuka daraja msimu wa 2025-2026 kwa kushika nafasi ya 16 na pointi tisa baada ya kushinda mechi mbili, sare tatu na kupoteza 25, kati ya 30, imeanza vizuri Ligi ya Championship, ikipambana ili kurejea tena katika Ligi Kuu Bara.

Kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini, Mbeya, wenyeji maafande wa Tanzania Prisons iliyoichapa Mbeya Kwanza ya Tabora mabao 2-1, itaikaribisha Mbuni FC ya Arusha, yenye mwenendo usioridhisha hadi sasa, baada ya kuchapwa mechi mbili mfululizo.

Mbuni FC yenye makazi yake jijini, Arusha, imeanza msimu vibaya baada ya kuchapwa mabao 5-1, dhidi ya kikosi cha KMC FC, kisha ikachapwa tena ugenini na Mtibwa Sugar mabao 2-1 na kuendelea kuburuza mkiani mwa nafasi ya 16, katika msimamo.

Maafande wa Tanzania Prisons walishuka daraja kupitia Play-Off, baada ya kumaliza nafasi ya 13 na pointi zao 32, huku ikicheza na kikosi cha Mbeya City kilichomaliza kikiwa nafasi ya 14 na pointi 30 na kutolewa kwa jumla ya mabao 2-0.

Baada ya hapo, timu hiyo ikacheza Play-Off nyingine ya kujinasua na janga la kushuka daraja dhidi ya Polisi Tanzania iliyoitoa Mbeya Kwanza kwa jumla ya mabao 7-1, kisha safari ya Prisons ikaishia hapo kwa kuchapwa jumla ya mabao 4-1.

MASTA 05

Mechi ya mwisho itapigwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini, Tabora ambapo Rhino Rangers iliyotoka suluhu (0-0), ugenini dhidi ya Songea United, itaikaribisha Mtibwa Sugar yenye kumbukumbu nzuri baada ya kuichapa Mbuni FC mabao 2-1.

Timu ya Rhino ni mabingwa wa Ligi Daraja la Kwanza kwa msimu wa 2025-2026, baada ya kuifunga Bandari Tanzania iliyopanda kwa kuongoza kundi A na pointi 32 kwa penalti 4-2, kufuatia sare ya kufungana mabao 2-2, mechi iliyopigwa Juni 17, 2026.

Rhino Rangers ilimaliza vinara wa kundi B na pointi 35 kwa msimu wa 2025-2026, baada ya kushinda mechi 11, sare mbili na kupoteza moja tu kati ya 14, iliyocheza huku kikosi hicho kikifunga mabao 31 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara tisa.

Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’, amesema ushindani huu umeanza mapema kutokana na maandalizi ya kila timu, jambo linaloonyesha wazi usipojipanga ni rahisi kudondosha pointi nyingi na kujiweka katika mazingira magumu.

“Tumecheza mechi mbili ngumu ugenini na kupata pointi tatu kati ya sita tulizotakiwa kuzipata, tunarudi tena nyumbani kwa mashabiki zetu, hivyo, ni lazima tuonyeshe heshima ya kupambana kutokana na umuhimu wao kwetu,” amesema Nsajigwa.