SALUM SUED KUSSY:Nyumbani kwake ni sebene tu
Muktasari:
Sued ni beki wa zamani wa Taifa Stars, Yanga na Mtibwa Sugar lakini kwa sasa yuko nyumbani akiuguza majeraha.
WATANZANIA wamezoea kumwona Salum Hamis Sued ‘Kussy’ anapokuwa uwanjani.
Hata hivyo, Mwanaspoti inakuletea maisha ya Sued ambaye ni maarufu pia kwa jina la Jibaba baada ya kufika nyumbani kwake, Mbezi, Makabe Mtaa maarufu unaoitwa Kwa Dunia.
Sued ni beki wa zamani wa Taifa Stars, Yanga na Mtibwa Sugar lakini kwa sasa yuko nyumbani akiuguza majeraha.
Alifanyiwa upasuaji wa enka ya mguu wa kushoto katika hospitali ya mifupa MOI wiki iliyopita na sasa yuko na P.O.P ambalo anatakiwa aondolewe baada ya mwezi kumalizika.
Sued ni miongoni mwa wachezaji wachache wanaoitwa baba mwenye nyumba. Anamiliki mjengo wake mwenyewe katika eneo hilo la Kwa Dunia, Mbezi, Makabe.
Kimtazamo ni nyumba nzuri, ambayo inajitosheleza kwa kila kitu, ipo katika mazingira tulivu, ambayo yatamfurahisha mgeni yeyote anatakayefika eneo hilo.
Safari ya kwenda Mbezi, Makabe haikuwa rahisi hasa kwa kuwa hali ya hewa ya sasa ni ya mvua.
Hata hivyo, mwandishi hakujutia safari yake kwani alifurahia mazingira aliyoyakuta.
Kwa mtazamo wa karibu utagundua kuwa ni nyumba yenye furaha kwani Sued na mke wake Vumilia Singu, wote wamejaa tabasamu wakati wote.
Maisha nyumbani
Mwanaspoti: Kwa nini ulichagua kujenga nyumba hapa?
Sued: Ni kwa sababu ndipo nilipobahatika kupata kiwanja.
Mwanaspoti: Unafurahia mazingira?
Sued: Kabisa, nafurahia sana maisha ya hapa nyumbani, kama unavyoona mazingira ni mazuri, hakuna vurugu kumetulia, huku kila mmoja anafanya mambo yake.
Mwanaspoti: Ni sehemu gani ya nyumba yako unaipenda?
Sued: Napenda zaidi chumbani, kule ndipo natuliza akili nalala, pia napanga mambo yangu mengine ya maendeleo nikiwa katika hali ya utulivu.
Mwanaspoti: Ni sehemu gani nje ya nyumba yako huwa unapenda kupumzika.
Sued: Mh, aisee sipendi kabisa kukaa nje. Kama nipo nyumbani mara nyingi napenda kukaa hapa sebuleni.
Mwanaspoti: Unapokuwa nyumbani unapenda kufanya nini?
Sued: Huwa napenda zaidi kusikiliza muziki.
Mwanaspoti: Muziki wa aina gani?
Sued: Napenda zaidi kusikiliza muziki wa Bolingo. Ninapotulia hapa, ni sebene tu, huwa nasikiliza za hapa nyumbani Tanzania pamoja na Congo.
Mwanaspoti: Shughuli gani ambazo unapendelea kufanya hapa nyumbani?
Sued: Ahaa, kwa kawaida, huwa nafanya shughuli zote kama kufua, kusafisha nyumba, lakini kupika ndiyo napenda zaidi.
Napenda sana kupika chakula na najua, nikikupikia lazima ufurahie. Napendelea kupika pilau au mchemsho wa samaki kwa sababu ndiyo chakula ninachopenda.
Mwanaspoti: Kitu gani ni muhimu zaidi katika maisha yako?
Sued: Familia. Familia yangu ndiyo kila kitu na ninaposema familia namaanisha, mke wangu, watoto, wazazi na ndugu wengine wote.