Safu ya ushambuliaji yaipasua kichwa Mlandege
Muktasari:
- Katika mchezo uliochezwa Septemba 4, 2026 kwenye Uwanja wa Mao A kisiwani Unguja, Mlandege ilifungwa mabao 2-0 na Polisi.
KOCHA Msaidizi wa Mlandege, Sabri China amesema udhaifu katika eneo la ushambuliaji pamoja na hofu iliyowakumba wachezaji wakati wa mchezo ni miongoni mwa sababu zilizochangia timu hiyo kupoteza dhidi ya Polisi.
Katika mchezo uliochezwa Septemba 4, 2026 kwenye Uwanja wa Mao A kisiwani Unguja, Mlandege ilifungwa mabao 2-0 na Polisi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Sabri amesema Mlandege haikutumia vizuri nafasi ilizopata jambo lililowafanya washindwe kupata mabao ambayo yangeweza kubadilisha mwelekeo wa mchezo. Amesema licha ya timu hiyo kuonyesha ushindani katika baadhi ya vipindi vya mchezo, eneo la mwisho lilikuwa tatizo kubwa kutokana na wachezaji kushindwa kufanya uamuzi sahihi walipofika lango la wapinzani.
Pia, amesema hofu ya mchezo iliathiri kiwango cha baadhi ya wachezaji, hususani katika nyakati ambazo walitakiwa kucheza kwa utulivu na kujiamini zaidi.
“Polisi walitumia hali hiyo kupata nafasi na kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kushambulia huku sisi Mlandege tukishindwa kurejea kwenye mpango wa awali wa mchezo,” amesema Sabri.
Amesema matokeo hayo yamewapa funzo na kwamba benchi la ufundi litafanyia kazi upungufu uliojitokeza katika umaliziaji na namna ya kuwajenga wachezaji kisaikolojia kabla ya michezo ijayo. Kocha huyo amesisitiza kuwa, Mlandege haiwezi kukata tamaa kutokana na kipigo hicho, akieleza kuwa lengo ni kurekebisha makosa, kuongeza kujiamini kwa wachezaji na kuhakikisha timu inarudi ikiwa imara zaidi katika mchezo unaofuata.
Mlandege ambayo imeshuka dimbani mara mbili katika Ligi Kuu Zanzibar msimu huu, imefanikiwa kukusanya pointi moja kufuatia kutoka sare ya mabao 3-3 dhidi ya JKU, huku ikopoteza mbele ya Polisi Zanzibar 2-0. Septemba 18, 2026, Mlandege itashuka dimbani dhidi ya Muembe Makumbi kwenye uwanja wa Mao A, Unguja.