Tatu zaanza kinyonge Ligi Kuu Zanzibar
Muktasari:
- Timu hizo ni Mwenge iliyopanda daraja msimu huu ambapo mechi mbili za kwanza ilizocheza, imepoteza zote. Nyingine ni KMKM na KVZ zilizocheza mechi moja.
WAKATI mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) ukikamilika Septemba 4, 2026, huku mzunguko wa tatu ukianza jana Jumapili, timu tatu zimeonekana kuanza kinyonge baada ya kushindwa kupata pointi.
Timu hizo ni Mwenge iliyopanda daraja msimu huu ambapo mechi mbili za kwanza ilizocheza, imepoteza zote. Nyingine ni KMKM na KVZ zilizocheza mechi moja.
KMKM na KVZ zilipoteza mechi ya kwanza ya ligi msimu huu, hivyo bado hazijacheza mechi za mzunguko wa pili kwani zina kazi ya kuiwakilisha Zanzibar kimataifa. KVZ inashiriki Ligi ya Mabingwa na KMKM ipo Kombe la Shirikisho Afrika.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa timu hizo tatu, Uhamiaji, Muembe Makumbi na Polisi zimefanikiwa kushinda mechi mbili za kwanza na kukusanya pointi sita kila moja, huku Uhamiaji ikifunga mabao matano na kuruhusu moja.
Hata hivyo, katika mizunguko hiyo miwili, Muembe Makumbi na Polisi ndiyo timu ambazo hazijaruhusu nyavu zao kutikiswa, huku kila moja ikifunga mabao matatu.
Katika hatua nyingine, kati ya timu nne zinazoshiriki ligi hiyo zikitokea kisiwani Pemba, Wembe pekee ndiyo iliyoonja ushindi ikiichapa Black Sailors mabao 2-0, huku Mwenge, Chipukizi na Fufuni bado zinajitafuta zikiambulia sare na vipigo.
Chipukizi imekuwa timu ya kwanza ZPL kuruhusu mabao mengi katika mechi moja baada ya kupokea kipigo cha mabao 4-1 kutoka kwa Uhamiaji, huku Mlandege ikiwa ndiyo timu iliyoruhusu mabao mengi kwa ujumla ambayo ni matano.
Katika mzunguko wa pili, yamefungwa mabao 15, ikiwa ni tofauti ya bao moja la mzunguko wa kwanza yalipofungwa 16, ikifanya idadi ya mabao hadi sasa kufikia 31.
Jana mzunguko wa tatu wa ligi hiyo ulianza ikiwa ni mwendelezo wa mapambano ya kumsaka bingwa wa 2026-2027.