Datius Peter wala hana presha Geita Gold
Muktasari:
- Datius ambaye amewahi kuzitumikia Stand United, Mbao FC, Kagera Sugar na Mtibwa Sugar kabla ya kujiunga na Geita Gold, alifichua hayo mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa Ligi Kuu Bara ambapo Geita Gold ilipoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Simba.
BEKI wa Geita Gold, Datius Peter, amesema hana presha anapokutana na wachezaji wenye ubora mkubwa, akieleza kuwa uzoefu wa kucheza Ligi Kuu kwa miaka tisa umemjengea kujiamini na uwezo wa kukabiliana na changamoto uwanjani.
Datius ambaye amewahi kuzitumikia Stand United, Mbao FC, Kagera Sugar na Mtibwa Sugar kabla ya kujiunga na Geita Gold, alifichua hayo mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa Ligi Kuu Bara ambapo Geita Gold ilipoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Simba.
Akizungumzia ugumu wa mchezo huo, Peter alisema ubora wa mawinga wa Simba uliwapa changamoto, lakini akaeleza kuwa baadhi ya makosa waliyofanya wenyewe ndiyo yaliwaathiri zaidi.
“Sipati presha yoyote kwa sababu najiamini na uzoefu ninao. Nikikutana na mpinzani wangu naona kawaida tu, kama ninavyokutana na wachezaji wengine, ila lazima nimuheshimu mpinzani wangu,” alisema.
Beki huyo alisema matokeo hayo hayajawapa presha kubwa, akisisitiza kuwa wanapaswa kujifunza ili mechi zinazofuata wafanye vizuri.
Geita Gold iliyorejea Ligi Kuu Bara msimu huu, tayari imecheza mechi tano ikishinda mbili na kupoteza idadi kama hiyo, huku ikitoka sare moja. Imekusanya pointi saba ikiwa nafasi ya sita kwenye msimamo.