Sababu Mrundi wa Fountain kutimka
Muktasari:
- Nyota huyo aliyejiunga na Fountain Gate, Agosti 1, 2024 akitokea Bumamuru ya kwao Burundi, amefikia uamuzi huo wa kuondoka na sasa anajiunga na mabingwa watetezi wa Kombe la Kagame mwaka 2026, Rayon Sports FC kutoka Rwanda.
ALIYEKUWA kiungo mshambuliaji wa Fountain Gate, Mrundi Elie Mokono amefikia uamuzi wa kuondoka ndani ya kikosi hicho, licha ya waajiri wake kumuwekea mkataba mpya wa miaka miwili wa kuendelea kuichezea, baada ya huu wa sasa kumalizika.
Nyota huyo aliyejiunga na Fountain Gate, Agosti 1, 2024 akitokea Bumamuru ya kwao Burundi, amefikia uamuzi huo wa kuondoka na sasa anajiunga na mabingwa watetezi wa Kombe la Kagame mwaka 2026, Rayon Sports FC kutoka Rwanda.
Chanzo kutoka kwa mtu wa karibu na mche- zaji huyo, kimeliambia Mwa naspoti, nyota huyo aliwekewa mkataba mpya wa miaka miwili ili aendelee kuichezea Foutain Gate, japo kutokana na klabu hiyo kufungiwa kusajili kwa msimu wa 2026-2027, akasitisha uamuzi wa kusaini.
“Uongozi ulitumia sana nguvu kubwa ya kumshawishi ila ikashindikana, alitaka wawalipe madeni wachezaji wote wanaowadai ili waruhusiwe kusajili, baada ya ukimya wa muda mrefu akasitisha mazungumzo ya kusaini mkataba,” kilisema chanzo hicho.
Katika msimu wake wa kwanza hapa nchini wa 2024-2025, nyota huyo alionyesha kiwango kizuri na kuanza kufuatiliwa na timu mbalimbali, baada ya kuifungia Fountain Gate mabao saba ya Ligi Kuu Bara, akiwa ndiye aliyefunga mengi kikosini humo.
Msimu wake wa pili ambao ni wa 2025-2026, akiwa na kikosi hicho, akashindwa kuendeleza kiwango chake baada ya kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara na kumaliza kwa kuchangia bao lake moja tu la Ligi Kuu Bara, kwa maana ya kutoa pia asisti.