Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ronaldo, Messi ni washikaji, ila lao moja- 3

Muktasari:

  • Uwapo wa mtu kama Messi umemfanya Ronaldo kupambana na kuwa katika kiwango cha juu zaidi cha ubora na Messi naye ana mtazamo wa aina hiyo hiyo.

KATIKA toleo lililopita mwandishi, Luca Caioli aligusia kauli za makocha wawili maarufu, Sir Alex Ferguson na Carlo Ancelotti, wote walionekana kumkubali Ronaldo wakidai kuwa ni zaidi ya Messi huku mashabiki wa wanasoka hao nao wakigawanyika. Endelea…

Wanapewa picha ya mastaa mahasimu wakubwa, kila mmoja akiwa na uwezo wa kuufunika ubora au ukubwa wa mwenzake, mashabiki na watu wa Ronaldo wakati wote wamekuwa wakikataa kwamba, Messi ni zaidi na ni hivyo hivyo kwa mashabiki wa Messi kwa Ronaldo.

Inapotokea mashabiki wao kokote duniani wanapoonyesha hasira zao humlinganisha mmoja dhidi ya mwenzake, na hata kwa vyombo vya habari, swali ambalo wamekuwa wakiulizwa sana ni lile la kutaka maoni ya mmoja dhidi ya mwenzake, Ronaldo ataulizwa maoni yake kuhusu Messi na Messi naye ataulizwa kuhusu Ronaldo.

Pamoja na yote hayo walau mbele ya hadhara wawili hao wameendelea kupeana heshima ya kiwango cha juu, “sisi ni washikaji. Ni marafiki ni profesheno ingawa hatuna tabia ya kukutana mara kwa mara nje ya uwanja wa soka, ni hivyo hivyo ulivyo urafiki wangu na wanasoka wenzangu wengine,’’ anaeleza Ronaldo.

“Anafanya juhudi ili kucheza soka katika ubora kadri awezavyo kwa klabu na nchi yake ni kama ambavyo mimi nafanya, kuna huo uhasama kwa maana ya kwamba sote tunataka kufanya kilicho bora kwa timu zetu, natumaini miaka michache ijayo tutarudisha kumbukumbu nyuma na kuanza kucheka pamoja.

“Soka ni mchezo, unahusisha burudani jambo linalotufanya tufurahi, ni kitu kizuri ambacho kila mtu duniani anakifurahia, ni lazima tulichukulia suala hili la uhasama katika namna nzuri kwa sababu ni jambo zuri.’’ Anamalizia Ronaldo.

Uwapo wa mtu kama Messi umemfanya Ronaldo kupambana na kuwa katika kiwango cha juu zaidi cha ubora na Messi naye ana mtazamo wa aina hiyo hiyo.

“Hakuna uhasama, hakujawahi kuwa na kitu kama hicho, ni jambo ambalo vyombo vya habari vinapenda kulikuza, sote tunataka kufanya mambo yetu katika ubora kadri iwezekanavyo kwa ajili ya klabu zetu, si suala la Messi na Ronaldo, haijawahi kuwa hivyo.” Anafafanua Messi.

Ukweli ni kwamba kidogo kulikuwa na hali ya presha siku za mwanzo mwanzo pale wachezaji hao wanapopishana katika mechi au hadharani. Lakini katika misimu ya karibuni wamekuwa wakiichukulia poa hali hiyo hata kupeana salamu za ishara kama ilivyokuwa wakati wa tuzo za mwanasoka bora wa dunia mwaka 2015.

Hali ya ukomavu imekuwa ikijitokeza uwanjani katika miaka ya karibuni duniani kote, lakini tusikosee kwamba wote hawa wanataka kitu kimoja, kila mmoja anataka mafanikio kumzidi mwenzake, wana hasira ya ushindi, wana hamasa katika hilo, ni wapambanaji wasiochoka katika hilo, wana msukumo wa kuwa bora kila wakati pamoja na ari ya kutaka mafanikio.

Kwa wakati wote wanaamini kuwa mafanikio yako katika uwezo wao na wanachohitaji ni kujiamini na shauku ya kufanikisha hilo, hakuna kati yao mwenye kukata tamaa, wanajua kwamba mafanikio yanahitaji nidhamu na kujitoa mhanga.

Kitu kimoja walichonacho chenye mfanano ni uwezo wa kuweka hisia zao pembeni na kujitoa asilimia 200 katika majukumu yanayowakabili, wana kipaji na ufundi, kwa ‘asili’ ni wafungaji wa mabao lakini pia ni watu profesheno ambao wametekwa katika hilo na wakati wote wanataka kufanya mambo kwa usahihi.

Nani bora kati yao, mwandishi Caioli katika kitabu hiki hajaribu kujibu swali hilo badala yake anakukupa kila kitu unachohitaji kukijua kuhusu wanasoka hawa mastaa na baada ya hapo utakuwa na uwanja mpana wa kuwa na jibu sahihi la nani zaidi ya mwenzake.

Itaendelea Jumamosi ijayo….