Prime
Ramani ya Simba CAF: Barker ashusha mikakati kabambe Malawi
KIKOSI cha Simba kimeanza safari ya kuifuata Mighty Wanderers FC ya Malawi katika mechi ya kwanza ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Steve Barker akiweka wazi mikakati kabambe ya ushindi.
Mechi hiyo itakayopigwa Jumapili ya Septemba 6, 2026, kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Bingu jijini Lilongwe, Malawi, ni ya awali kusaka tiketi ya kwenda hatua ya pili na baadaye kufuzu makundi, huku timu zote zikihitaji kufikia malengo hayo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Barker amesema maandalizi ya mechi hiyo yamekamilika kwa kiwango kikubwa na wachezaji wote wana morali ya kupambana ugenini, licha ya kukiri ugumu anaoenda pia kukutana nao kutokana na ubora wa wapinzani wao.
“Ni mechi muhimu kwetu kwa sababu tunahitaji kuendeleza mwenendo mzuri, haitokuwa rahisi kutokana na aina ya mpinzani tunayecheza naye, ni timu yenye muunganiko mzuri wa kiuchezaji, hivyo ni lazima tuchukue tahadhari,” amesema Barker.
Aidha, Barker amesema kucheza na timu yenye muunganiko mzuri na isiyotegemea mchezaji mmoja ni ngumu sana kupambana nayo katika hatua hii, ingawa maandalizi yaliyofanyika hadi sasa kwa kikosi hicho yanawapa matumaini ya kufanya vizuri zaidi.
“Mechi zetu tano za Ligi Kuu Bara tulizocheza zimetuongezea motisha ya kupambana, malengo yetu ni kuhakikisha mechi hii ya ugenini tunafanya vizuri kwa maana ya kupata ushindi mzuri, utakaoondoa presha tutakapocheza hapa nyumbani.
“Tunafahamu hakuna mchezo rahisi, lakini tumeshawasoma wapinzani wetu na tunafahamu vitu vingi kuhusu wao, mambo yanaweza kubadilika lakini ukweli ni kwamba tunakwenda kutafuta ushindi na siyo sare,” amesema.
Mara ya mwisho Simba kucheza kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Bingu, iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Nyasa Big Bullets ya Malawi, Septemba 10, 2022, yaliyofungwa na nyota Mzambia Moses Phiri dakika ya 30 na John Bocco dakika ya 84.
Mechi hiyo ilikuwa ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo msimu huo wa 2022-2023, Simba ilishinda nyumbani mabao 2-0, Septemba 18, 2022, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na kufuzu kwa jumla ya mabao 4-0.
Katika Ligi Kuu Bara msimu huu, Simba imeshinda mechi zote tano ilizocheza ikiwa na pointi 15, sawa na Yanga ambayo inaongoza kwa tofauti ya mabao, huku pia Mighty Wanderers ikishika nafasi ya pili na pointi 29 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Malawi.
Katika Ligi Kuu ya Malawi (TNM Super League), pointi 29 za Mighty Wanderers ni sawa na za Silver Strikers inayoongoza kwa tofauti ya mabao, baada ya kikosi hicho kucheza mechi 14, kikishinda nane, sare tano na kupoteza moja tu.
Msimu wa 2025-2026, Simba iliishia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa mkiani mwa kundi D na pointi tano, nyuma ya Petro de Luanda kutoka Angola iliyomaliza nafasi ya tatu na pointi sita, Esperance de Tunis ya Tunisia iliyomaliza nafasi ya pili na pointi tisa, huku Stade Malien ya Mali ikiongoza na pointi 11, katika mechi sita.
Malengo ya Simba ni kufika nusu fainali msimu huu wa 2026-2027, ikisaka rekodi mpya tangu mara ya mwisho kwake ilipofika mwaka 1974, ambapo kwa wakati huo michuano hiyo iliitwa Klabu Bingwa Afrika.
Simba inakwenda kwenye mchezo huu ikiwa na kikosi kipya kwa asilimia kubwa tofauti na kile ambacho kilicheza michuano hiyo msimu uliopita,