Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Raha ya ngoma ujue mapigo yake!

Muktasari:

Baada ya kutuma habari nilipumzika Hoteli ya Kilimanjaro Native Cooperative Union (KNCU) na nikiwa nimelala nilisikia mlango unagongwa.

YAPO mambo siwezi kuyasahau katika maisha yangu ya zaidi ya miaka 50 ya uandishi wa habari kuanzia nilipokaribia kumaliza masomo Shule ya Msingi.

Miongoni mwao ni wakati nilipoandika habari za michezo ya ndani na nje ambayo niliicheza tokea nikiwa shule. Hii ni pamoja na gofu, mpira wa magongo na kriketi na ya vijiweni kama karata, bao na dhumna. Katika siku za mwisho za 1969 au mwanzoni wa 1970, sina uhakika wa tarehe, nilikwenda Moshi, kutoka Arusha palipokuwa makao yangu nikiwa Mwandishi wa Gazeti la Standard (sasa Daily News).

Kilichonipeleka Moshi ni kuandika habari za kuwekwa jiwe la msingi la Hospitali ya Kilimanjaro Christian Medical Centre (KCMC).

Baada ya kutuma habari nilipumzika Hoteli ya Kilimanjaro Native Cooperative Union (KNCU) na nikiwa nimelala nilisikia mlango unagongwa.

Nilipofungua niliwakuta waandishi wa habari niliofanya kazi nao Arusha, Patrick Makomu wa magazeti ya Uhuru na Nationalist na marehemu Richard Msaky wa Idara ya Habari.

Kilichowaleta kilinishangaza kutokana na kuniuliza watu wa Zanzibar ni wa aina gani. Nilipowauliza sababu waliyonieleza ilinishangaza.

Msaky aliniambia timu ya mpira wa Magongo kutoka Zanzibar kwa mashindano yaliyofanyika Moshi yakiwa na timu za Tanzania, Kenya na Uganda ilikuwa sio ya kawaida ilikuwa na sura tafauti na walizozizoea katika mchezo huo, yaani haikuwa na Wahindi, Wazungu wala Magoha.

Niliwaeleza hiyo ndio Zanzibar na ndio maana waliniona mara nyingi Arusha nikicheza kriketi na gofu.

Baadaye nilitambua sio wao tu walioshangazwa. Siku ya pili niliona watu wengi walifika uwanjani sio kuona kama kweli Waswahili wa Zanzibar walikuwa na uweledi wa mchezo huo wa magongo.

Watu walivutiwa kuona timu ya Zanzibar ikiwa na mchanganyiko wa wachezaji, wakiwemo wa umri wa miaka 16, kama Islam Ahmed Islam na wenye umri wa zaidi ya miaka 30 kama Abdul Majham na Maulidi Machaprala.

Wengine ninaowakumbuka katika timu ile ni Zaghalul Ajmi na ndugu yake, Ahmed Himidi Mbaye na kaka yake Babechi, Abdulla Pakistani na Ahmed Juma.

Mshangao ule ulinikumbusha nilipokuwa Dar es Salaam miezi michache baada ya kuhamishwa kutoka Zanzibar na Gazeti la Standard mwaka 1966.

Nilikumbana na mkasa ambao katika Lugha ya Waswahili inakwenda sambamba na msemo wa jamii ya Wahindi wa ‘Jamatini kaingia Golo’.

Neno golo linamaanishwa kuingia Mswahili ambaye hakutarajiwa kuwepo Jamatini. Kwa lugha ya siku hizi huyo aliyeitwa ni sawa na kumueleza kuwa ‘sio mwenzetu’.

Wakati ule walikuwepo watu wawili katika Standard walioandika habari za kriketi na mpira wa magongo.

Mmoja ambaye ni Goha alitumia jina la utani la ‘Flotsam’ na mwengine ni Gupta, Singa Singa ambaye ni daktari maarufu wa meno.

Siku moja wote hawakupatikana kuandika habari za kriketi. Flotsam alikuwa safarini na Gupta asingeweza kuandika kwa vile alikuwa mchezaji.

Baada ya majadiliano ofisini nilijitolea kwenda Uwanja wa Kinondoni kuandika habari za mchezo ule na viongozi wangu ofisini ambao ni Waingereza ningeweza kufanya hivyo.

Nilipofika Kinondoni nilikwenda kwenye banda la wachezaji na waamuzi na hapo ikazuka hadithi ya watu kuambizana Jamatini kaingia Golo.

Hawakuamini nilikuwa na uweledi wa mchezo kwani wakati ule watu waliokuwa karibu na michezo wa mpira wa magongo na kriketi nchini walikuwa Wazungu na Wahindi.

Watazamaji na wachezaji walishangaa kuniona na kitabu changu cha Uandishi wa Habari nikitafuta maelezo ya wachezaji na mashindano.

Waliona nilikuwa ninatania.

Kiongozi mmoja aliniambia isingewezekana kwa vile kriketi ni tafauti na kandanda niliokuwa mara nyingi naandikia habari zake katika gazeti.

Nilitabasamu na kumueleza sio nilikuwa ninajua kuandika habari za kriketi tu, bali pia ni mchezaji.

Alishangaa nilipomtajia wachezaji maarufu duniani wa zama zile kama Gary Sobers wa Carribean, Pataudi wa India na wachezaji maarufu wa Zanzibar kama Sherali Ndege na historia ya mashindano maarufu duniani ya Ashes.

Mtoto mmoja wa Sherally aliyekuwepo uwanjani na rafiki zake Bashir Tejani, Mohammed Nathoo na Sajjad Lakha kutoka Zanzibar ambao waliokuwa wachezaji wa timu ya Ithnaasheri (Union) walicheka.

Mwanamichezo maarufu wa Visiwani Said Nyanya aliyekuwa kiongozi wa Union alipoona jamaa hawaamini kama niliujua mchezo wa kriketi aliwaambia ninauelewa vizuri.

Sherally alisogea na kuwaambia si ajabu kwa sababu shule za mjini Zanzibar kabla ya Mapinduzi ya 1964 zilikuwa na timu za kriketi na wengi wa wachezaji walikuwa Waswahili.

Wale Wahindi waliozaliwa Dar es Salaam walipigwa na butwaa waliposikia habari ile na nilipowaambia Wahindi wa Zanzibar wa wakati alicheza bao na kuwinda ndege na njiwa kwa manati, tafauti na wao wa Bara walishangaa zaidi.

Niliwambia jamaa wa Kihindi kutoka Zanzibar waliokuwepo kwamba kufika kwangu pale kuandika habari za kriketi ilikuwa ni ile hadithi ya Jamatini kaingia golo.

Walicheka na Nathoo alitia mkono mfukoni, akakinipa tambuu na kuniambia nikitafuna hawataniona sio golo bali mwenzao.

Nilimwambia ahsante kwani sijawahi kutumia uraibu ule, japo mmoja wa mabibi zangu alikuwa mtumiaji mzuri wa tambuu.

Wakati wa mapumziko mashabiki waliniuliza, ilikuwaje nikaujua mchezo wa kriketi?

Nilipochambua mchezo kwa kuwaambia nahodha wa timu iliyoelemewa alichelewesha kumuingiza mrushaji mpira wa mizunguko (spinner) na kutumia mrushaji mipira ya wastani (medium pace bowler) inayomruhusu mpigaji kufyatua makombora kirahisi wakamini golo alikuwa anajua kriketi.

Hii ni moja ya kumbukumbu iliyoniganda kichwani kila nikifika Dar es Salaam na kwenda kuangalia kriketi na hukumbuka: Jamatini kaingia Golo.

Ninafarijika kuona siku hizi Tanzania tunao vijana wengi wanaoandika habari za michezo hii tafauti na zamani ambapo wengi walichofanya ni kutoa maelezo ya nani kashinda na sio kuchambua mchezo.

Ni vizuri habari za michezo mengine zikapewa umuhimu kama kandanda ili kushajiisha vijana wengi kushiriki michezo hii.