Kudunda afichua jambo TMA FC
Muktasari:
- TMA FC, ambayo ilitokea jijini Arusha na kuhamishia makazi yake Iringa baada ya kununuliwa, imekuwa na mwanzo mgumu wa msimu. Hadi sasa imeshinda mchezo mmoja, kutoka sare mbili na kupoteza sita, ikiwa mkiani mwa msimamo wa ligi katika nafasi ya 16 ikiwa na pointi tano.
KOCHA Msaidizi wa TMA FC ya Iringa, Ramadhan Kudunda, amesema ukosefu wa uzoefu kwa wachezaji wengi wa kikosi hicho ni miongoni mwa sababu zinazoifanya timu hiyo kufanya vibaya katika Ligi ya Championship msimu huu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kudunda amesema wachezaji wengi wa TMA FC hawana uzoefu wa kutosha wa mashindano hayo, hali inayochangia timu kushindwa kupata matokeo mazuri hadi sasa, tofauti na baadhi ya wapinzani wao ambao wamewekeza zaidi katika kuimarisha vikosi vyao.
“Wachezaji wetu si wazoefu kwa sababu wanatoka katika kituo cha Young Stars ambacho kinashiriki Ligi ya Mkoa wa Iringa. Kwa hali ya namna hiyo, ni ngumu sana kushindana. Tunachotaka kwa sasa ni kupambana tusishuke daraja,” amesema Kudunda.
Kocha huyo, ambaye amewahi kuzifundisha Lipuli FC ya Iringa, Tunduru Korosho na Majimaji FC ya Songea, amesema bado ni mapema kukata tamaa kutokana na mwenendo huo, akisisitiza kuwa wataendelea kupambana ili kuhakikisha wanamaliza vizuri mzunguko wa kwanza.
TMA FC, ambayo ilitokea jijini Arusha na kuhamishia makazi yake Iringa baada ya kununuliwa, imekuwa na mwanzo mgumu wa msimu. Hadi sasa imeshinda mchezo mmoja, kutoka sare mbili na kupoteza sita, ikiwa mkiani mwa msimamo wa ligi katika nafasi ya 16 ikiwa na pointi tano.