Prisons yaanza na askari ikisuka upya kikosi chake
Muktasari:
- Prisons ilishuka daraja msimu uliopita 2025-2026 baada ya kumaliza Ligi Kuu nafasi ya 13 kwa pointi 32 na kuangukia play off ambapo haikuweza kujitetea.
Wakati Tanzania Prisons ikijiandaa na msimu ujao wa Ligi ya Championship, timu hiyo imeanza kusuka upya kikosi chake kwa kuwafanyia majaribio askari wa Jeshi la Magereza ili kupata wachezaji watakaoongeza nguvu.
Prisons ilishuka daraja msimu uliopita 2025-2026 baada ya kumaliza Ligi Kuu nafasi ya 13 kwa pointi 32 na kuangukia play off ambapo haikuweza kujitetea.
Play off ya kwanza ilifungwa na Mbeya City jumla ya mabao 2-0, kisha ikaja kuchapwa jumla ya mabao 4-1 dhidi ya Polisi Tanzania iliyokuwa Ligi ya Championship.
Timu hiyo chini ya Kocha Mkuu, Shadrack Nsajigwa, imeanza kusuka upya kikosi chake kwa kufanya majaribio hayo katika mzoezi yaliyodumu kwa siku mbili yakishirikisha zaidi ya wachezaji 50.
Akizungumza baada ya mazoezi hayo, Nsajigwa amesema mkakati wao ni kuona timu inarudi Ligi Kuu akieleza kuwa baada ya mchujo huo wataongeza wengine wenye uwezo na uzoefu.
Amesema kwakuwa timu hiyo ni ya taasisi ya Jeshi, wanatumia mazoezi hayo kutafuta wachezaji wenye uwezo watakaoungana na wengine kwa ajili ya msimu ujao, akieleza kuwa ameona vipaji ni vingi.
"Tutapata wachezaji wasiopungua 30 japo watakuwa wanachujwa huko mbele, malengo ni kurejesha timu Ligi Kuu kutokana na mipango yetu, program imekuwa nzuri na tumeona vipaji.
"Tutakaowapata wataungana na wengine kwakuwa wapo ambao hawakuwa na timu ila wana vipaji, tutaendelea nao kuwanoa ili kutengeneza timu bora na yenye ushindani, lengo ni kurudi Ligi Kuu," amesema kocha huyo.
Tanzania Prisons katika ushiriki wake wa Ligi Kuu, ilisifika kuwa na soka la nguvu maarufu 'pira gwaride' ikiwa na nyota wengi waliokuwa askari akiwamo Jumanne Elfadhir, Samson Mbangula, Dotto Shaban, Lambert Sabiyanka, Jeremia Juma na Salum Kimenya.
Matarajio ya uongozi wa timu hiyo, mashabiki na wadau wa soka jijini Mbeya ni kuona kurejea kwa mfumo wa kuwatumia wachezaji ambao ni askari inaweza kurejesha uhai mpya wa Tanzania Prisons katika medani za soka nchini.