PRINCE DUBE: Huyu jamaa ni zaidi ya moto
Muktasari:
WAKATI anatambulishwa ndani ya Azam hakuna aliyemchukulia kwa uzito mkubwa. Kwanza ni kutokana na muonekano wa sura yake na hata umbile lake lilivyo. Hakutisha sana kama alivyo, Meddie Kagere wa Simba au Michael Sarpong au Yacouba Songne wanaokipiga Yanga.
WAKATI anatambulishwa ndani ya Azam hakuna aliyemchukulia kwa uzito mkubwa. Kwanza ni kutokana na muonekano wa sura yake na hata umbile lake lilivyo. Hakutisha sana kama alivyo, Meddie Kagere wa Simba au Michael Sarpong au Yacouba Songne wanaokipiga Yanga.
Hata alipoanza kutupia kambani, kuna mashabiki waliomchukulia poa. Waliamini amebahatisha tu na mbele ya safari moto wake ungezimika. Walimchukulia ni kama wachezaji wengine wakigeni waliosajiliwa na klabu hiyo walioanza na moto wa kifuu. Yahya Mohammed aliyesajiliwa kutoka Ghana. Alianza na moto kisha akapoa kabla ya kutemwa akiwa na mabao machache kabisa. Sitaki kuwataka wengine kadhaa ambao wamekuwa wakisumbuliwa na jinamizi la Kipre Tchetche. Straika nyota wa zamani aliyeacha alama ndani ya mabingwa hao wa zamani wa Tanzania na Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup). Kipre alijua kufunga bwana si mchezo. Enzi zake kila ulipokuwa ukisikia imooo basi lazima awe ametupia.
Namzungumzia Prince Dube, straika matata wa Azam FC kutoka Zimbabwe. Prince Dube anatisha. Anawaliza mabeki na makipa kwa namna anavyofunga mabao yake kibabe. Mpaka sasa jamaa keshafunza jumla ya mabao 14, akizidi kumuacha mbali mtetezi wa kiatu cha dhahabu, Meddie Kagere wa Simba. Jamaa ni moto mkali, ila basi tu, hatajwi labda kwa vile anakipiga timu isiyokuwa na mashabiki wengi kama Simba na Yanga.
Ebu chungulia rekodi zake chache kwenye dondoo hizi zinazoletwa na Mwanaspoti kuonyesha jamaa ni zaidi ya balaa!
TIMU 10 HOI
Kama hujui ni kwamba Mzimbabwe huyo mpaka sasa ameshaziliza jumla ya timu 10 kati ya 10 zinazochuana na Azam kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu.
Dube alianza mbio zake za kutupia kambani Septemba 11, 2020 alipoizamisha Coastal Union kwa mabao 2-0, yote akiyafunga mwenyewe. Moja alilitupia dakika ya 69 na jingine la 89 na kuwatia gundu Wagosi wa Kaya walioanza msimu na kipigo hicho kilichokuwa cha pili kwao.
Baada ya hapo Dube akapitiwa na ukame wa mabao kabla ya kuzinduka kwenye mechi ya ugenini mjini Sumbawanga, Azam ilipoifuata Tanzania Prisons na kuitungua bao 1-0 lililowekwa na Mzimbabwe huyo dakika ya 90 katika mechi iliyopigwa Septemba 26.
KAGERA
WANYONGE
Kama kuna timu ambayo imegeuzwa wanyonge mbele ya Dube basi ni Kagera Sugar, kwani ndiyo pekee iliyotunguliwa mara mbili msimu huu, akianza kuwaliza katika meechi iliyopigwa Okt 04, 2020 na kuzamishwa kwa mabao 4-2.
Dube alifunga mawili dakika ya 6’ na 88’, huku mengine yakiwekwa kimiani na Obrey Chirwa dakika ya 48’ na Richard Djodi dakika ya 51’.
Pia alikuwa kuiliza kwenye mchezo wa marudiano uliopigwa Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba siku ya Mar 03, 2021, ambapo bao lake lilikuwa la pili na la ushindi baada ya awali Raphael Brayson kuitanguliza Azam na baadaye wenyeji kupata penalti iliyozamishwa na Peter Mwalyanzi na matokeo kuwa mabao 2-1.
NYINGINE
ZILIZOUMIA
Okt 15, 2020, Azam iliialika Mwadui kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam na kuifumua mabao 3-0 na Dube alitupia moja dakika ya 61, wakati mengine yakiwekwa na Mzambia Obrey Chirwa katika dakika za 27’ na 63. Baadaye fundi huyo wa mpira alikuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na jeraha la mkono alilolipata kwenye mchezo wao dhidi ya Yanga ambao Azam ililala 1-0.
Aliporejea tena mapema mwaka huu, alikuja na moto mkali na urejeo wake ulianzia kwa kuitungua Mbeya City katika mechi iliyopigwa Feb 18 mwaka huu. Straika huyo alifunga bao lake dakika ya 29 baada ya Idd Seleman ‘Nado’ kutangulia dakika ya nne, huku bao la kufutia machozi la Mbeya likifungwa na beki wake, David Mwasa dakika ya 69.
Ndipo akaitungua Kagera Sugar na baada ya hapo akawanyoosha Mtibwa Sugar waliovaana nao Apr 09. Dube alifunga mara mbili na kuizamisha mabingwa hao wa zamani wa nchi kwa mabao 2-0. Kisha akarudi tena kambani kwa kufunga bao moja katika sare ya 2-2 dhidi ya Dodoma Jiji katika mechi iliyopigwa mjini Dodoma siku ya Apr 22, 2021.
Siku tatu baadaye, Dube akawatia njaa Yanga kwa kufunga bao pekee na la ushindi katika mechi kali iliyopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa. Dube alifunga bao tamu la mbali dakika chache kabla ya mchezo kumalizika na kuipotezea dira Yanga katika mbio zake za kuwania ubingwa.
Timu nyingine zinakamilisha idadi ya timu 10 zilizotunguliwa na Dube ni KMC waliocharazwa mabao 2-1 wikiendi iliyopita. Katika mchezo huo uliopigwa Mei 15, Dube alifunga bao la kuongoza kabla ya KMC kusawazisha kupitia Abdul Hilal na Agrey Morris kufunga bao la ushindi dakika za jioni kabisa.
Juzi usiku, Dube tena aliendeleza moto na kutimiza bao lake la 14 katika Ligi Kuu Bara msimu huu wakati wakiinyoa Biashara United kwa mabao 2-0. Dube alifunga tena bao la kwanza kabla ya kiungo fundi, Mudathir Yahya kufunga la pili.
SABA
ZANUSURIKA
Timu saba pekee ambazo Dube hajazitungua, ikiwamo Simba, JKT Tanzania, Ihefu SC, Ruvu Shooting, Polisi Tanzania, Gwambina na Namungo, kwani kwenye mechi za duru la kwanza baadhi alizikosa kwa kuwa majeruhi na nyingine walimdhibiti.
Hata hivyo habari mbaya kwa timu hizo ni kwamba, Azam ina michezo minne kabla ya kukamilisha msimu na baadhi ya timu hizo itakutana nazo, ikiwamo Simba, Gwambina, Namungo na Ruvu Shooting.
Kama timu hizo hazitajipanga na moto mkali wa Dube, wanaweza kulizwa naye, kwani jamaa ni kama anataka sifa kwa jinsi anavyotupia kambani.
Usichokijua ni kwamba katika mabao yake 14 ni moja tu ndio katupia kambani kwa mkwaju wa penalti, alipoiziamisha Mtibwa, lakini yaliyosalia ni ya juhudi zake binafsi akifunga kwa kichwa na ya miguu yake kuonyesha alivyo hatari.