Polisi yaimarisha ulinzi Kariakoo Dabi
Muktasari:
- Akizungumza na waandishi wa habari jana Oktoba 8, 2026, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Faustine Mafwele amesema maandalizi ya kiusalama yamefanyika kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwa ajili ya mechi hiyo.
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeimarisha ulinzi kwa ajili ya mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Simba na Yanga itakaochezwa kesho Jumamosi, Oktoba 10, 2026 kwenye Uwanja wa Uhuru.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Oktoba 8, 2026, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Faustine Mafwele amesema maandalizi ya kiusalama yamefanyika kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwa ajili ya mechi hiyo.
“Tunatambua uwepo wa mechi ya soka ya Ligi Kuu Bara itakayofanyika Jumamosi, Oktoba 10, 2026 katika Uwanja wa Uhuru ulioko Temeke, Dar es Salaam,” amesema Mafwele.
Mchezo huo wa msimu wa 2026/27, utawakutanisha watani wa jadi wa soka nchini, Simba na Yanga, huku Simba ikiwa mwenyeji wa pambano hilo linalotarajiwa kuanza saa 1:00 usiku.
“Ulinzi na usalama umeimarishwa kwa kushirikiana na wadau wote, wakiwamo mashabiki, wapenzi na wadau wote wa soka,” amesema.
Mafwele amesema jeshi hilo limeweka msisitizo katika kuhakikisha mashabiki wanazingatia sheria, kanuni na taratibu wakati wa kuelekea uwanjani, wakati wa mchezo na baada ya pambano kumalizika.
“Tunawakumbusha kujiepusha na vitendo vyote vile ambavyo viko kinyume na sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa ligi, lakini pia kinyume na taratibu za mikusanyiko katika mechi hii kubwa,” amesema.
Mechi hiyo inatarajiwa kukusanya idadi kubwa ya mashabiki wa timu hizo mbili kutokana na ukubwa wa dabi hiyo inayovuta hisia za mashabiki ndani na nje ya Dar es Salaam.
Mbali na ushindani wa pointi za ligi, mechi hiyo ni sehemu ya ratiba ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2026/27, huku Simba ikitumia Uwanja wa Uhuru kama wa nyumbani.
Katika mechi hiyo, mchakato wa ununuzi wa tiketi umeanza kwa mfumo wa kidijitali unaotumika kwa mechi za soka, huku mashabiki wakitakiwa kuutumia kupata tiketi zao badala ya kutegemea mauzo yasiyo rasmi.
Mfumo huo unawawezesha mashabiki kuchagua tiketi na maeneo ya kukaa kabla ya kufanya malipo, huku Uwanja wa Uhuru ukiwa na viti vyenye namba.
Mafwele amesema usalama wa mechi hiyo ni jukumu la pamoja kati ya vyombo vya ulinzi na usalama, waandaaji, klabu, mashabiki na wadau wengine wa soka.
“Nazitakia Simba na Yanga mechi nzuri na kuwataka mashabiki wa timu hizo kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha dabi hiyo inafanyika kwa amani na utulivu.”