Polisi SC watakiwa kuongeza umakini
Muktasari:
- Kauli hiyo ameitoa Agosti 26, 2026 katika uwanja Mao Zedong kisiwani Unguja wakati akizungumza na viongozi, wachezaji na benchi la ufundi wa timu hiyo.
MWENYEKITI wa Polisi SC ya Zanzibar, Kamishna Msaidizi wa Polisi, ACP Omar Khamis Abdalla, ameikumbusha timu hiyo kuongeza umakini kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Zanzibar 2026-2027.
Kauli hiyo ameitoa Agosti 26, 2026 katika uwanja Mao Zedong kisiwani Unguja wakati akizungumza na viongozi, wachezaji na benchi la ufundi wa timu hiyo.
Amewataka wachezaji kutimiza wajibu wao kwa kupambana na kuonesha kiwango kizuri kwani mashabiki wanaimani na timu hiyo na wanatarajia kuona matokeo mazuri uwanjani na si vinginevyo.
“Nahitaji wachezaji pamoja na benchi la ufundi kuongeza juhudi, umakini na kujituma katika maandalizi ya michezo ya Ligi Kuu Zanzibar msimu wa 2026-2027,” amesema.
Mwenyekiti huyo amewataka wachezaji na benchi la ufundi kuwa na umoja, nidhamu na kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuhakikisha timu inafikia malengo.
“Mashabiki wana imani na nyinyi, hivyo ni wakati wa kujipanga, kupambana na kuhakikisha tunawapa furaha kwa matokeo mazuri,” amesema.
Amesema, msimu uliopita timu hiyo haikufanya vizuri, hivyo amewataka wachezaji na benchi la ufundi kurejesha heshima ya Polisi iliyokuwa na historia nzuri Ligi Kuu.
Polisi SC katika msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar msimu uliopita 2025-2026 ilishika nafasi ya 11 ikikusanya pointi 41 baada ya kucheza mechi 30, ikishinda 12, sare tano na kupoteza 13.
Polisi SC ilimaliza nafasi ya pili kutoka mstari mwekundu wa kushuka daraja msimu uliopita.