Zanzibar yasuka mikakati ya AFCON 2027
Muktasari:
- Kamishna Idara ya Mipango na Maendeleo ya Kisekta kutoka Tume ya Mipango Zanzibar, Mohamed Massoud Salim, alisema maandalizi yanalenga kukuza uchumi, kuongeza ajira na kuimarisha huduma za kijamii.
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imeendelea kuweka mikakati ya kuonesha ipo tayari kuwa mwenyeji wa Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2027) kwa kuboresha miundombinu ya michezo na usafiri.
Kamishna Idara ya Mipango na Maendeleo ya Kisekta kutoka Tume ya Mipango Zanzibar, Mohamed Massoud Salim, alisema maandalizi yanalenga kukuza uchumi, kuongeza ajira na kuimarisha huduma za kijamii.
Alisema, Serikali inaimarisha huduma za afya, usalama na usafiri kukabiliana na ongezeko la wageni linalotarajiwa kwenye michuano hiyo.
“Zanzibar kuwa mwenyeji wa AFCON inatoa fursa ya kuongeza shughuli za uchumi hususani katika sekta ya utalii, usafiri na biashara ndogondogo,” alisema.
Vilevile, alisema AFCON inahitaji maandalizi ya Serikali, sekta binafsi na wadau wengine kuhakikisha huduma zinakidhi viwango.
Alisema uwekezaji unaofanywa na Serikali kwa maandalizi hayo una manufaa na maslahi mapana ya nchi kwa siku zijazo.
Aliongeza kuwa, Serikali inaangalia namna bora ya kuongeza ushiriki kwa wananchi kutumia fursa hiyo katika shughuli za kiuchumi.
Kuanzia Juni 19, 2027 hadi Julai 17, 2027, michuano hiyo itafanyika kwa nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), timu zitakazopangwa kituo cha Tanzania, mechi zake zitapigwa Dar es Salaam, Arusha na Zanzibar.