Polisi, JKU zavimbiana Ligi Kuu Zanzibar
Muktasari:
- Katika kipindi cha kwanza, safu ya ushambuliaji ya Polisi ilionekana kupeleka mashambulizi mengi kwenye ngome ya Polisi, lakini mlinda mlango wa timu hiyo pamoja na mabeki walikuwa imara.
TIMU za Polisi na JKU, zimeshindwa kutambiana baada ya kutoka suluhu katika mchezo mkali wa kusisimua wa Ligi Kuu ya Zanzibar (ZPL) uliopigwa Uwanja Mao A, Unguja, Novemba 20, 2026.
Mchezo huo uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka visiwani hapa, ulianza kwa kasi huku timu zote mbili zikishambuliana kusaka bao la mapema la kuongoza.
Katika kipindi cha kwanza, safu ya ushambuliaji ya Polisi ilionekana kupeleka mashambulizi mengi kwenye ngome ya Polisi, lakini mlinda mlango wa timu hiyo pamoja na mabeki walikuwa imara.
Kwa upande wa JKU, ilijibu mashambulizi kupitia mipira ya kushtukiza ambapo ilitengeneza nafasi nyingi za wazi lakini ilishindwa kuzimalizia.
Licha ya timu hizo kutengeneza nafasi kwa vipindi vyote, lakini washambuliaji wao walikosa utulivu wa kutumbukiza mpira wavuni jambo ambalo lilichangia mechi hiyo kumaliza bila kufungana.
Mbali kasi ya mchezo kuongezeka na presha kupanda kadiri muda ulivyokuwa ukiyoyoma, ngome za timu zote mbili ziliendelea kuwa imara na kuhakikisha hakuna nyavu zinazotikishwa hadi mwamuzi alipopuliza filimbi ya mwisho.
Matokeo hayo yanazifanya timu hizo kugawana alama moja moja, hatua inayozifanya kuendelea kukabana koo kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Timu ya JKU imeendelea kusalia nafasi ya pili ya msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 27, wakati Polisi yenye pointi 26 ipo nafasi ya tatu, huku Zimamoto ikiendelea kushika usukani wa ligi hiyo kwa pointi 31.