Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dakika 15 zilivyowavuruga Serengeti Boys

DAKIKA Pict

Muktasari:

Ukitazama matokeo peke yake unaweza kupongeza ari ya vijana wa Kocha Elieneza Nsanganzelu ya kurejesha mabao mawili ya mapema kwa takwimu Tanzania haikupata pointi moja tu bali ilipoteza pointi mbili muhimu zilizokuwa mkononi mwake.
 

TAKWIMU hazidanganyi ndio unavyoweza kusema baada ya Timu ya Taifa ya wavulana U-17, Serengeti Boys baada ya kupata sare ya mabao 2-2 dhidi ya Costa Rica kwenye mechi ya kundi I ya Kombe la Dunia iliyopigwa Uwanja wa Aspire Zone (Pitch 1) jijini Doha, Qatar.

Ukitazama matokeo peke yake unaweza kupongeza ari ya vijana wa Kocha Elieneza Nsanganzelu ya kurejesha mabao mawili ya mapema kwa takwimu Tanzania haikupata pointi moja tu bali ilipoteza pointi mbili muhimu zilizokuwa mkononi mwake.


DAKI 04

DAKIKA 15 ZA MWANZO

Tanzania iliingia uwanjani ikionekana kuwaheshimu kupita kiasi wapinzani wao Costa Rica wanaoshiriki fainali hizi kwa mara ya 12, huku Serengeti ambao ni wageni wakicheza mara ya kwanza.

Ndani ya dakika 15 tu, safu ya mabeki ilikuwa imeshakubali mabao mawili. Bao la kwanza la Jefrey Urbina dakika ya 8 lilitokana na viungo wa kati kuchelewa kuziba njia nje ya boksi, na kumpa nafasi ya kupiga shuti la chini lililojaa wavuni.

Dakika saba baadaye, uzembe wa kucheza faulo isiyo na ulazima nje ya eneo la hatari kwa kipa Haji Abdallah ukampa Jorshuad Pilarte fursa ya kufunga bao la pili kwa mpira wa adhabu.


KUTAWALA BILA MIPANGO

Kipindi cha pili, Tanzania iligeuka kuwa mwiba kwa Costa Rica. Kocha Nsanganzelu alifanya mabadiliko ya kimbinu kwa kumwingiza Bashiri Kibaila kuchukua nafasi ya Luqman Mbalasalu dakika ya 46, mabadiliko yaliyoongeza uhai na kasi kwenye eneo la ushambuliaji ambapo hata wakati Tanzania ikipokokwa mpira ndani ya sekunde 20 vijana hao wanapokonya na kwenda kushambulia kwa wapinzani.

Takwimu zinaonyesha Tanzania ilimiliki mpira kwa asilimia 59, ikapiga pasi sahihi 316 (asilimia 77) na kutengeneza mashuti 25 huku mashuti 18 yakipigwa ndani ya boksi la Costa Rica.

Hata hivyo, safu ya ushambuliaji haikuwa na ubora eneo la mwisho. Kati ya mashuti 25, ni matano tu ndiyo yaliyolenga lango, huku mashuti 14 yakipaa na kutoka nje!

Mfano ni mshambuliaji nyota, Faraji Kayanda. Licha ya kufunga mabao yote mawili dakika ya 51 kwa pasi ya Razaki Mbegelendi na dakika ya 73 kwa kichwa kutokana na mpira wa kutenga wa Kibaila, Kayanda ndiye aliyepoteza nafasi ya wazi nyingi zaidi alipokosa mkwaju wa penalti dakika ya 55.

Kama angekuwa mtulivu kwenye penalti ile na nafasi nyingine mbili alizopata ndani ya boksi, leo tungeshuhudia hat-trick ya kihistoria na ya pili kwenye michuano hiyo hadi sasa.

Nidhamu ya ukabaji na kadi za mapema pia ilikuwa tatizo, Tanzania ilijikuta ikipoteza mwelekeo katika dakika 10 za mwisho kutokana na faulo nyingi zisizo za lazima ikicheza faulo 11 zilizosababisha kadi tatu za njano kwa Haji Abdalah (14’), Hussein Mbegu (47’) na Kassim Juma (59’). Kadi hizi ziliwafanya mabeki kucheza kwa tahadhari kubwa badala ya kuendelea kuwasukuma Costa Rica nyuma.


DAKI 03

NINI KIFANYIKE?

Sare dhidi ya Costa Rica inaiweka kwenye mtego mkubwa Tanzania kuelekea mechi ya pili dhidi ya mabingwa mara nne wa dunia, Brazil (Novemba 24, saa 9:00 alasiri), ambao wana washambuliaji hatari kama Eduardo Conceição na Rodrigo Júnior.

Ili Tanzania isiambulia kipigo kitakachowatoa mchezoni mapema, benchi la ufundi linapaswa kufanya mambo manne ya haraka.

Kwanza, Kufuta hali ya woga. Brazil wanapenda kumaliza mechi ndani ya dakika 20 za mwanzo. Tanzania lazima ianze mchezo ikiwa na umakini mkubwa tangu filimbi ya kwanza, tofauti na ilivyoanza dhidi ya Costa Rica.

Pili nidhamu ya kuzuia nje ya boksi. Costa Rica waliiadhibu Serengeti mabao yote mawili kutokana na mashuti na faulo za nje ya boksi (walipiga mashuti nane nje ya boksi dhidi ya moja tu ndani ya boksi).

Brazil wana mafundi wa kupiga mashuti ya mbali na mipira iliyokufa; viungo wa chini Issa Chole, Hamis Mihambo na Idrisa Kilendemo lazima wafunge njia zote za katikati na kuepuka faulo za kizembe karibu na eneo la penalti.

Tatu mabadiliko kwenye safu ya ushambuliaji: Kwa kuwa Brazil wamezoea kumiliki mpira muda mwingi, Tanzania haiatakuwa na mwaya wa kupata nafasi 25 kama ilivyokuwa kwa Costa Rica kutokana na ubora wa safu ya wapinzani wake.

Kwenye nafasi mbili au tatu za mashambulizi ya kushtikiza ambazo Tanzania inaweza kuzipata angalau itumie moja ili kuepuka madhara ya kujutia baadae.

Kocha anapaswa kumpa nafasi ya kuanza Bashiri Salum Kibaila ambaye alileta uhai mkubwa alipoingia kipindi cha pili na kutengeneza bao la kusawazisha.

Nne kutumia mipira iliyokufa. Bao la pili la Tanzania lilipatikana kupitia mpira wa adhabu. Dhidi ya timu kubwa kama Brazil, mipira ya kona na faulo ndiyo silaha rahisi zaidi ya kupatia pointi. Kama Serengeti Boys itaweza kuziba mianya ya mapema na kutumia vyema nafasi chache watakazopata, wanaweza kuushangaza ulimwengu mjini Doha.


DAKI 01

MSIKIE KOCHA

Kocha Nsanganzelu anasema kwa namna kikosi kilivyocheza walistahili kuondoka na ushindi wa pointi tatu akimini nafasi zilizotengezwa.

“Ni mechi ambayo tulishahili kupata kila kitu hawa bado wachezaji wadogo na wanaendelea kujifunza, hatuwezi kuwalaumu tunaendelea kuwapa moyo ili kuwa na umakini mwanzoni,” amesema

“Nadhani wachezaji walikuwa na presha ya mashindano mwanzoni lakini tulikuwa bora sana tulitengeneza nafasi nyingi na tulistahili kufunga mabao mengi.”


DAKI 02

KAYANDA AANDIKA HISTORIA

Mshambuliaji wa timu hiyo,  Kayanda ameandika historia kwa kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Tanzania kufunga mabao mawili katika michuano hiyo.

Nyota huyo anayekipiga Dodoma Jiji, alionyesha kiwango bora kwa kufunga mabao hayo dakika ya 51 na 73.

Kayanda anakuwa mchezaji wa kwanza kwa upande wa wanaume kutoka Tanzania kufunga mabao mawili katika mashindano hayo, ambayo ni mara ya kwanza kushiriki Kombe la Dunia la vijana chini ya miaka 17.

Kwa upande wa wanawake, Diana Mnally ndiye aliyekuwa nyota wa kwanza wa Tanzania kuweka historia ya kufunga katika Kombe la Dunia baada ya kupachika bao dakika ya 17.

Tanzania ilishinda 2-1 dhidi ya Ufaransa, Oktoba 15, 2022, kwenye Kombe la Dunia la Wasichana U-17 lililofanyika India.

Katika michuano hiyo, Serengeti Girls iliandika historia ya kucheza robo fainali ya Kombe la Dunia.

Bao la Mnally lilipatikana katika hatua ya makundi, ambapo Tanzania ilipangwa Kundi D pamoja na Japan, Canada na Ufaransa.

Japan iliongoza kundi hilo, Tanzania ikamaliza nafasi ya pili, huku Canada na Ufaransa zikishika nafasi za tatu na nne.

Sasa Kayanda anaendeleza historia hiyo kwa upande wa wanaume. Licha ya kufunga mabao mawili yaliyoirudisha Serengeti Boys mchezoni, mshambuliaji huyo alikosa penalti dakika ya 55 iliyomfanya ashindwe kufunga hat trick.

Kiwango alichoonyesha katika mchezo huo pia kilimfanya kuweka historia nyingine ya kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Tanzania kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mechi.

Hata hivyo, licha ya mabao hayo, mshambuliaji huyo wa Dodoma Jiji angeweza kuongeza idadi ya mabao kama angetumia vizuri nafasi alizotengeneza.

Kwa kufanya hivyo, angekuwa mchezaji wa pili kufunga hat-trick kwenye michuano hiyo baada ya Halidou Maïga wa Mali, aliyefunga mabao matatu katika ushindi wa 3-0 dhidi ya New Zealand, Novemba 20, 2026.

Akizungumzia mchezo huo baada ya kumalizika, Kayanda amesema: “Namshukuru Mungu kwa mara ya kwanza tumeshiriki mashindano na mimi binafsi kupata kile ambacho nimejiwekea kwenye mashindano haya. Tulikuwa na nafasi ya kufanya vizuri zaidi, lakini hatutakata tamaa na mimi binafsi pia nitapambana mechi ijayo,” amesema.