Picha linaanza Sasa yanga
Muktasari:
- BENCHI la ufundi la Yanga pamoja na mashabiki jana walikuwa na furaha iliyoje baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya JKT Tanzania uliowarudishia mzuka wa mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
BENCHI la ufundi la Yanga pamoja na mashabiki jana walikuwa na furaha iliyoje baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya JKT Tanzania uliowarudishia mzuka wa mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, mashabiki wa Yanga walikuwa wakitamba kwamba; “Sasa dozi ziendelee na aje anayefuata.”
Mabao ya Yanga kwenye mchezo huo uliokuwa na kasi ya aina yake, yalifungwa na Yacouba Sogne na Tuisila Kisinda na kuifanya Yanga kuwa pointi sawa na Simba kileleni.
Yanga wamecheza mechi 29 na kufikisha pointi 61 sawa na Simba, lakini wanakuwa wa pili kwenye msimamo kutokana na uwiano wa mabao ya kufunga na kufunga ambao Simba wanayo ya kumwaga. Simba wamecheza mechi 25 wakiwa tofauti ya michezo minne na Wananchi.
Wakati Yanga wakipunguza gepu la pointi, mshambuliaji Yacouba Sogne anakuwa kinara wa mabao kikosini baada ya kufunga bao moja kwenye ushindi huo akifikisha magoli saba na kumpita Deus Kaseke mwenye sita.
Katika kipindi cha kwanza Yanga ya Kocha Nasredine Nabi ilionyesha kuhitaji bao la kuongoza lakini mastraika walikuwa na papara huku JKT wao wakitumia zaidi mipira ya pembeni na staili ya kupiga mipira mirefu kuhakikisha wanaipenya safu ya ulinzi ya Yanga lakini wakatulizwa.
Dakika 12 mshambuliaji, Danny Lyanga wa JKT Tanzania alipiga shuti kali kutokea nje ya 18 lakini umahiri kipa wa Yanga, mzawa Metacha Mnata aliucheza mpira huo na kuwa kona isiyokuwa na faida na kumfanya ashangiliwe mpaka na vigogo wa jukwaa kuu.
Yanga walijibu shambulizi dakika 25 na Yacouba Sogne alifunga kwa kichwa bao la kuongoza akiunganisha vizuri krosi ya Kibwana Shomari na kuinua mashabiki wa Yanga ambao baadhi yao walisafiri kutoka mikoani.
Bao hili liliwarejesha mchezoni Yanga iliyokuwa imepanga mziki wote, baada ya mchezo uliopita kutoka sare tasa dhidi ya Namungo na kuwanyong’onyesha wachezaji hao.
Dakika 28 Edward Songo alionyeshwa kadi ya njano baada ya kumfanyia madhambi Saido Ntibazonkiza nje kidogo na boksi la JKT Tanzania iliyosaliwa na pointi zake 33 kwenye msimamo wa Ligi.
Yanga ilipata bao la pili na la ushindi dakika 30 kupitia kwa Mkongomani anayesifika kwa kutoka nduki, Tuisila Kisinda baada ya winga, Ditram Nchimbi aliyepiga krosi ya chinichini huku mabeki wa JKT wakashindwa kuuzua mpira huo na kukutana na mfungaji aliyetupia kambani. Kosa hilo la mabeki lilizua mzozo zaidi kwenye benchi la JKT ambao walionekana kunyoosha vidole uwanjani.
Dakika 39 JKT Tanzania walifanya shambulizi baada ya mshambuliaji Rashid Mandawa kugongeana na Shaban Mgandila ambaye alipiga shuti la kishikaji ambalo halikuwa na madhara likatoka nje ya goli.
JKT walikuwa wanatumia zaidi kupita katika upande wa mabeki wa kushoto na kulia, Michael Aidan na Edson Katanga lakini krosi zao zilikuwa zinaishia kwa beki wa Yanga, Bakari Mwamnyeto.
Kufanikiwa kucheza vema kwenye eneo la kiungo cha Yanga, kilichoongozwa na Mukoko Tonombe na Feisal Salum, kiliipa uhakika mkubwa Yanga kuwavuruga na kuwatawala JKT Tanzania.
Maafande JKT, walijitutumua bila mafanikio kuwafunga Yanga, huku kukosa umakini kwenye eneo la ulinzi kuliwagharimu.
Mbali na yote, tofauti na mechi zilizopita za Simba dhidi ya JKT Tanzania na ule dhidi ya Dodoma Jiji, ambao mashabiki walifurika uwanjani, hali ilikuwa tofauti kwa mchezo huu.
Mashabiki hawakuwa wengi kwa sehemu kubwa ya majukwaa kuwa tupu kuanzia VIP B, C na yale ya mzunguko.
Ushindi wa jana umewaongezea faraja Yanga kwani bado unawabakiza kwenye mbio za ubingwa huku wakimuombea mabaya mtani wao Simba ambaye ana akiba kubwa ya mechi nne mkononi. Kama Yanga wangeterereka na kupoteza jana ilimaanisha kwamba Simba walikuwa na mlima mdogo wa kushinda mechi japo tano mfululizo tu kutetea ubingwa wao kwenye Ligi.
Mechi nyingine iliyopigwa jana, Gwambina iliyoko bado kwenye mstari wa uwezekano wa kushuka daraja na kurudi kwenye Ligi Daraja la Kwanza, wakiwa kwao walilazimishwa suluhu na Namungo yenye sare 10 kama Tazania Prisons.