Mtibwa Sugar yasaka bosi mpya
Muktasari:
- Timu hiyo ya mkoani Morogoro ilishuka daraja msimu wa 2023/24, kisha kurejea Ligi Kuu msimu wa 2025/26 ambapo ilishuka tena na sasa msimu ujao wa 2026/27 itacheza Championship.
MTIBWA Sugar imesema kushuka daraja mara mbili mfululizo imewaumiza sana akili, ikiahidi kufanya tathimini ya utulivu kupanga safu mpya ya uongozi na kuimairisha kikosi kwa ajili ya msimu ujao.
Timu hiyo ya mkoani Morogoro ilishuka daraja msimu wa 2023/24, kisha kurejea Ligi Kuu msimu wa 2025/26 ambapo ilishuka tena na sasa msimu ujao wa 2026/27 itacheza Championship.
Ofisa Habari wa timu hiyo, Thobias Kifaru amesema matokeo ya kushuka daraja mara mbili mfululizo yamewaumiza sana uongozi ikilinganishwa na ukubwa na historia ya timu hiyo kwenye medani za soka nchini.
Amesema kwa sasa hawatakuwa na uharaka wa kusuka timu badala yake watafanya tathimini ya kina kubaini kilichowaangusha hata kama watatumia muda mrefu, lakini wapate suluhisho la kudumu.
“Tunafikiria kwanza kupata Ofisa Mtendaji Mkuu ambaye atatupeleka kwenye mafanikio ya muda mrefu kama ilivyokuwa huko nyuma chini ya Jamal Bayser, tunaendelea kufanya tathimini ya kina kujua tumekosea wapi”
“Inaumiza Mtibwa Sugar, timu bora, yenye uchumi, historia na rekodi kubwa kwenye soka ndani na nje kuona tunapata matokeo haya ya kuumiza, hatutakurupuka bali tutatuliza akili kupata kiongozi wa mafanikio ya muda mrefu” amesema Kifaru.
Ofisa huyo ameongeza kuwa watakuwa tayari kuchelewa kufanya usajili kwa lengo la kumpata mtu sahihi wa kuivusha timu katika kipindi hiki kigumu, akieleza kuwa kwakuwa wanao uwezo wa kulipa mishahara, usajili wanaweza kufanya hata siku moja wakamaliza.
Kuhusu wachezaji wanaoondoka kikosini humo baada ya timu kushuka, Kifaru amesema hawatamzuia yeyote kuondoka badala yake wataangalia namna ya kutengeneza kikosi chao kipya kitakachowapa mafanikio ya mbeleni.
“Kama timu ina uwezo mathalani kulipa Sh 5 milioni, kwanini tusiweze kusajili hata kwa siku moja, hatutazuia yeyote kuondoka, tunaweza kutengeneza timu ya mbeleni hata tukichelewa” amesema Ofisa huyo.
Katika mafanikio ya Mtibwa Sugar ni kubeba ubingwa wa Ligi Kuu kwa miaka miwili mfululizo ikifanya hivyo 1999 na 2000, huku ikitwaa taji la kombe la shirikisho (kwa sasa CRDB) msimu wa 2020/21.