Geita Gold yawinda staraika Mcongo
Muktasari:
- Nyota huyo amefikia makubaliano ya kutoongeza mkataba mpya na waajiri wake wa zamani wa Namungo FC, baada ya kukitumikia kikosi hicho cha ‘Wauaji wa Kusini’ kwa misimu mitatu, tangu alipojiunga nayo kwa mara ya kwanza kwa msimu wa 2023-2024.
BAADA ya Namungo FC ‘Wauaji wa Kusini’, kuachana rasmi na aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo raia wa DR Congo, Fabrice Ngoy, uongozi wa Geita Gold umeanza mazungumzo ya kumsajili nyota huyo ili kuongeza nguvu katika eneo la ushambuliaji.
Nyota huyo amefikia makubaliano ya kutoongeza mkataba mpya na waajiri wake wa zamani wa Namungo FC, baada ya kukitumikia kikosi hicho cha ‘Wauaji wa Kusini’ kwa misimu mitatu, tangu alipojiunga nayo kwa mara ya kwanza kwa msimu wa 2023-2024.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ngoy amesema baada ya kuachana na Namungo kuna timu mbalimbali anazoendelea kufanya nazo pia mazungumzo kwa ajili ya kujiunga na moja kati ya hizo, japo, ni mapema kuweka wazi kwa sababu hakuna makubaliano rasmi.
“Kwa sasa nipo nyumbani DR Congo na ninaendelea na mazungumzo na baadhi ya timu na tukifikia makubaliano nitajiunga na moja kati ya hizo, malengo yangu ni kuendelea kucheza tena katika Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2026-2027,” amesema Ngoy.
Kwa upande wa Ofisa Habari na Mawasiliano wa Geita Gold, Samwel Dida amesema licha ya ukimya wa timu hiyo ila mashabiki wa kikosi hicho watarajie usajili mzuri kwa ajili ya msimu wa 2026-2027, kutokana na maboresho makubwa yaliyofanyika.
“Kwa sasa tunaendelea na mazoezi yetu Morogoro na muda wowote tutaanza kuwatangaza wachezaji wetu wapya watakaoongeza nguvu na wengine tutakaoachana nao, mambo mazuri mbeleni yanakuja na mashabiki zetu watajionea wenyewe,” amesema Dida.
Ngoy alijiunga na Namungo msimu wa 2023-2024, akitoka Kitayosce iliyobadilishwa jina na kuitwa Tabora United na sasa TRA United, baada ya kuifungia mabao 15 ikiwa Ligi ya Championship, nyuma ya kinara, Edward Songo wa JKT Tanzania aliyefunga 18.
Mshambuliaji huyo alitua hapa nchini kwa mara ya kwanza msimu wa 2022-2023, akitokea Real Nakonde FC ya Zambia na msimu wa 2023-2024, alifunga bao moja tu la Ligi Kuu Bara, huku 2024-2025, akifunga mawili na msimu wa 2025-2026, amefunga mabao 11.