Pesa zamuondoa Diana Cherono Ceasiaa
Muktasari:
- Diana, ambaye msimu uliopita alikuwa sehemu ya kikosi cha Ceasiaa Queens, amesajiliwa na Kibera baada ya klabu hiyo kuweka mezani ofa yenye masilahi makubwa zaidi kwa mshambuliaji huyo.
MSHAMBULIAJI raia wa Kenya, Diana Cherono ameondoka Ceasiaa Queens ya Tanzania na kutua Kibera Soccer Women FC ya Kenya, huku suala la fedha likitajwa miongoni mwa sababu zilizochangia kutoendelea kusalia kikosini humo.
Diana, ambaye msimu uliopita alikuwa sehemu ya kikosi cha Ceasiaa Queens, amesajiliwa na Kibera baada ya klabu hiyo kuweka mezani ofa yenye masilahi makubwa zaidi kwa mshambuliaji huyo.
Aliyekuwa Kocha wa Ceasiaa Queens, Ezekiel Chobanka amesema mkataba wa Diana na klabu hiyo ulikuwa umetamatika, hivyo Kibera Soccer Women FC ilipofika na dau kubwa, lilifanya iwe vigumu kwao kumbakiza.
“Mkataba wake ulikuwa unaisha na Kibera walikuja na pesa ndefu, hilo lilifanya iwe vigumu kumbakiza Tanzania,” amesema Chobanka.
Diana amejiunga na Kibera akiwa na rekodi nzuri katika soka la wanawake nchini Kenya, baada ya awali kuitumikia Vihiga Queens na kuonyesha kiwango kikubwa katika mashindano ya ndani.
Mshambuliaji huyo alitwaa tuzo ya mfungaji bora Kenya msimu wa 2024-2025. Mbali na mafanikio ya klabu, Diana pia amewahi kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Kenya, Harambee Starlets mwaka 2024, hivyo anaingia Kibera akiwa na uzoefu wa kucheza katika kiwango cha kimataifa.
Kibera Soccer Women FC imeamua kumpa jukumu hilo la kuongeza makali katika safu yake ya ushambuliaji baada ya msimu uliopita kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu.