Pesa ilivyoimaliza Simba Sauzi
Muktasari:
MATOKEO ya Simba kufungwa mabao 4-0 na Kaizer Chiefs katika mechi ya mkondo wa kwanza wa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika yanaweza kuwa uthibitisho tosha wa namna fedha inavyoweza kukupa kile ambacho wengi hawakitegemei.
MATOKEO ya Simba kufungwa mabao 4-0 na Kaizer Chiefs katika mechi ya mkondo wa kwanza wa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika yanaweza kuwa uthibitisho tosha wa namna fedha inavyoweza kukupa kile ambacho wengi hawakitegemei.
Wachezaji wa Kaizer Chiefs ambao walitoa mchango mkubwa katika kikosi chao hadi kuibuka na ushindi huo mnono ni wale ambao ni vinara katika chati ya nyota wa timu hiyo wanaolipwa kiasi kikubwa cha fedha
Samir Nurkovic aliyefunga mabao mawili katika mchezo huo, ndiye mchezaji anayelipwa kiasi kikubwa cha fedha kwani kwa mwezi analipwa kitita cha Randi 950,000 zaidi ya Sh 152 milioni kwa mwezi, fedha ambayo inaweza kuwa mshahara wa takribani wachezaji 10 au zaidi wa Simba.
Katika kikosi hicho, wachezaji watano kati ya saba wanaoongoza kwa kulipwa kiasi kikubwa cha fedha ndani ya timu hiyo walicheza.
Mwanaspoti linakuletea orodha ya nyota saba wa Kaizer Chiefs wanaolipwa mshahara mkubwa kwa mwezi;
1.Samir Nurkovic- Randi 950,000 (Sh 152 milioni)
Nyota huyo raia wa Serbia mwenye umri wa miaka 28 ambaye aliifunga mabao mawili, alisajiliwa na Kaizer Chiefs kutokea timu ya Komarno inayoshiriki Ligi Daraja la Pili huko Serbia.
Ndiye anayeoongoza kwa kulipwa mshahara mkubwa katika kikosi cha Kaizer Chiefs.
2.Khama Billiat-Randi 830,000 (Sh 133.6 milioni)
Mzimbabwe huyo mwenye umri wa miaka 30, hakucheza mechi dhidi ya Simba kutokana na kukabiliwa na majeraha
3.Itumeleng Khune- Randi 480,000 (Sh 77.8 milioni)
Ndiye nahodha wa timu hiyo ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 33. Hakucheza mechi dhidi ya Simba juzi kutokana na majeraha.
4. Lebogang Manyama- Randi 300,000 (Sh 48.3 milioni)
Kiungo mshambuliaji wa timu hiyo ambaye aliisumbua vilivyo Simba katikati mwa uwanja na katika safu yao ya ulinzi kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuchezesha timu na kupika mashambulizi.
Ndiye alipika bao la tatu kwa kupiga pasi iliyookolewa vibaya na Mohamed Hussein na kuunganishwa na Samir Nurkovic
5. Bernard Parker-Randi 300,000 (Sh 48.3 milioni)
Ndiye mchezaji mwenye umri mkubwa kwenye kikosi hicho akiwa na umri wa miaka 35 na ndiye alipiga kona iliyozaa bao la kwanza la timu hiyo katika mchezo wa dhidi ya Simba.
6.Eric Mathoho- Randi 220,000 (Sh 35.4 milioni)
Ameifungia jumla ya mabao matatu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu likiwemo moja dhidi ya Simba.
7. Willard Katsande-Randi 200,000 (Sh 32.2 milioni)
Nyota huyo wa Zimbabwe mwenye umri wa miaka 35, katika mchezo dhidi ya Simba, aliingia dakika ya 86 kuchukua nafasi ya Njabulo Blom.