Pamba Jiji yakaribia kunasa straika
Muktasari:
- Nyota huyo aliyeibuka mfungaji bora katika Ligi Kuu ya DR Congo (Linafoot Ligue 1) msimu wa 2025-2026, wakati akiwa na kikosi cha AS Dauphins Noirs alichokifungia mabao 21, amejiunga na Singida Black Stars ingawa atatolewa tena kwa mkopo.
KLABU ya Pamba Jiji iko katika hatua za mwisho za kufikia makubaliano ya kumsajili mshambuliaji, Mkongomani Candidat Mapendo kwa mkopo akitokea Singida Black Stars, baada ya kikosi hicho cha ‘TP Lindanda’ au ‘Wanakawekamo’ kumuhitaji.
Nyota huyo aliyeibuka mfungaji bora katika Ligi Kuu ya DR Congo (Linafoot Ligue 1) msimu wa 2025-2026, wakati akiwa na kikosi cha AS Dauphins Noirs alichokifungia mabao 21, amejiunga na Singida Black Stars ingawa atatolewa tena kwa mkopo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Pamba, Ezekiel Ntibikeha amesema kuna mazungumzo yanaendelea na nyota mbalimbali ili kupata saini zao, baada ya kupokea ripoti ya benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Mkenya Francis Baraza.
“Wachezaji wote tuliowatambulisha ni wale tuliofikia makubaliano nao, wapo wengine ambao bado hatujakubaliana ila muda wowote tutakamilisha pia usajili wao na kuwatangaza rasmi katika kurasa zetu za mitandao ya kijamii,” amesema Ntibikeha.
Mwanaspoti linatambua, sababu kubwa ya Singida kumtoa Mapendo kwa mkopo ni kutokana na kuzidi kwa idadi ya wachezaji 12 wa kigeni wa kikosi hicho, huku ikiamini Pamba Jiji itakuwa sehemu nzuri pia ya kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara.
Mbali na Mapendo ila Pamba Jiji iko katika hatua nzuri pia za kuipata saini ya mshambuliaji mwingine raia wa DR Congo, Malanga Horso Mwaku kutoka Singida Black Stars kwa mkopo, baada ya kuamua kuachana naye kwa ajili ya kusajili wengine. Singida Black Stars imekamilisha usajili wa wachezaji wanne kutokea Pamba Jiji.