Pamba Jiji, Dodoma Jiji zaanza kwa sare
Muktasari:
- Dodoma Jiji ndiyo ilianza kufunga bao kupitia winga Beno Ngassa aliyefunga dakika ya 17, akiweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga msimu huu.
MECHI ya kwanza ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2026-2027, iliyochezwa leo Ijumaa Agosti 14, 2026 kati ya wenyeji Pamba Jiji dhidi ya Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, imemalizika kwa sare ya bao 1-1.
Dodoma Jiji ndiyo ilianza kufunga bao kupitia winga Beno Ngassa aliyefunga dakika ya 17, akiweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga msimu huu.
Hata hivyo, Pamba Jiji haikuwa nyuma kwani ilijibu mashambulizi na kusawazisha dakika ya 24 kupitia mshambuliaji Deogratius Mafie na kuzipeleka timu hizo mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.
Kipindi cha pili kilionekana kuwa na mashambulizi ya kila upande huku kila timu ikisaka bao la ushindi, lakini hadi dakika tisini zinatimia, hakuna iliyofanikiwa.
Matokeo ya mchezo huo yamezifanya timu hizo kuanza msimu huu kwa kugawana pointi moja.
Hata hivyo, katika mchezo wa mwisho wa msimu uliopita uliozikutanisha timu hizo Mei 10, 2026, zilitoka suluhu.
Sare hiyo imekuwa mwanzo wa safari mpya kwa Pamba Jiji baada ya kumaliza msimu uliopita ikiwa katika nafasi ya saba ikikusanya pointi 36 kutokana na michezo 30, ikishinda tisa, sare tisa na kupoteza 12.
Dodoma Jiji nayo imeanza msimu kwa kupata pointi moja, baada ya kumaliza msimu uliopita ikiwa na matokeo yasiyoridhisha katika michezo yake ya mwisho, ikiwemo kupoteza 0-2 dhidi ya Azam FC na kufungwa mabao 0-5 na Singida Black Stars. Ilimaliza nafasi ya tisa ikikusanya pointi 35 baada ya kushinda mechi nane, sare 11 na kupoteza 11.
Baada ya mchezo wa leo, Pamba Jiji inatarajiwa kuendelea na kampeni yake Agosti 19, 2026 kwa kuikaribisha Simba, wakati Dodoma Jiji ikiifuata Mbeya City siku hiyohiyo kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.