Nyota IAA SC aota ufungaji bora
Muktasari:
- Mshambuliaji huyo aliyecheza KenGold, Ndanda na Mbeya City chini ya miaka 20, kisha, Chitipa United ya Malawi, amesema moja ya jambo linalompa matumaini ya kufanya vizuri ni kufundishwa na Kocha, Maka Mwalwisi aliyekuwa naye Mbeya Kwanza.
MSHAMBULIAJI mpya wa IAA SC ya jijini, Arusha, Boniface Mwanjonde amesema miongoni mwa malengo yake msimu huu akiwa na kikosi hicho ni kuibuka mfungaji bora katika Ligi ya Championship, licha ya kukiri ushindani mkubwa wa kuwania nafasi.
Nyota huyo amejiunga na timu hiyo inayoshiriki Ligi ya Championship kwa mara ya kwanza msimu huu wa 2026-2027, baada ya kuachana na kikosi cha Mbeya Kwanza cha mjini Tabora, ambacho kwa msimu uliopita wa 2025-2026, alikifungia mabao 11.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mwanjonde amesema licha ya kuichezea timu hiyo kwa mara ya kwanza, ila atapambana na kuleta ushindani kwa washambuliaji wenzake, huku akipigania malengo ya kuibuka mfungaji bora baada ya kushindwa akiwa Mbeya Kwanza.
"Licha ya malengo ya timu kucheza Ligi Kuu Bara ila mengine ni yangu binafsi ya kuibuka mfungaji bora, natambua wazi ni ngumu kutokana na aina ya ushindani uliopo katika Ligi ya Championship, japo kwangu naichukulia ni fursa mpya," amesema.
Mshambuliaji huyo aliyecheza KenGold, Ndanda na Mbeya City chini ya miaka 20, kisha, Chitipa United ya Malawi, amesema moja ya jambo linalompa matumaini ya kufanya vizuri ni kufundishwa na Kocha, Maka Mwalwisi aliyekuwa naye Mbeya Kwanza.