Nsajigwa alia na mpiga penalti
Muktasari:
- Hii ni baada ya kukosa mabao ya pigo hilo kwenye mechi mbili mfululizo wakianza na Mtibwa Sugar kwenye kipigo cha bao 1-0 na ile ya ushindi wa mabao 2-1 mbele ya Transit Camp katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
ACHANA na matokeo mazuri waliyonayo Tanzania Prisons, Kocha Mkuu wa timu hiyo Shedrack Nsajigwa amesema kwa sasa anaumiza kichwa kumpata mpiga penalti maalumu kikosini kutokana na kuandamwa na mzimu wa kukosa mapigo hayo.
Hii ni baada ya kukosa mabao ya pigo hilo kwenye mechi mbili mfululizo wakianza na Mtibwa Sugar kwenye kipigo cha bao 1-0 na ile ya ushindi wa mabao 2-1 mbele ya Transit Camp katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Katika mechi hizo, mchezaji Oscar Paul alikosa mkwaju wa penalti kwenye mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar huko mkoani Morogoro, huku Othman Ochu akikosa mbele ya Transit Camp
Prisons iliyoshuka daraja msimu uliopita imeonekana kuwa na mwenendo mzuri kwenye Championship kutokana na kuwa nafasi ya nne kwa pointi 13 baada ya kucheza mechi saba.
Akizungumza na Mwanaspoti, Nsajigwa amesema kutokana na mzimu huo kuwaandama, anaenda kutengeneza mfumo mpya wa kumpata mchezaji maalumu wa matukio hayo ili kuendana na kasi ya ligi.
Amesema wakati wanaanza msimu hawakufanya jambo hilo, hali inayoanza kuwapa ugumu huku akiwapongeza nyota wake wanavyopambana kutafuta pointi tatu.
“Awali hatukuwa na mpiga penati, lakini kutokana na mwenendo huu lazima tulifanyie kazi kuwa na mtu maalumu, kwa ujumla matokeo si mabaya sana japokuwa kuna namna tunapaswa kupambana”
“Championship ni jina tu lakini ushindani wake, mbinu na uwezo wa makocha ni kama Ligi Kuu, ndio maana timu inapata matokeo popote bila kujali unacheza na nani, hiki tunakizingatia sana” amesema.