Nikiwa na Amasha, Madaraka tuliibeba Fanja FC ya Oman
Muktasari:
Wakati alifafanua aliichezea Small Simba hadi Machi,1984 alipokwenda nchini Oman kucheza soka la kulipwa na tofauti na wengine ambao huingia mikataba na vilabu, yeye alipelekwa moja kwa moja katika kambi ya Timu ya Taifa ya Oman.
WIKI iliyopita, tuliona jinsi Small Simba ilivyobadilisha fikra za watu kutoka kushabikia Simba na Yanga hadi timu hiyo, Malindi na zingine za Unguja na Pemba, sasa endelea…
Wakati alifafanua aliichezea Small Simba hadi Machi,1984 alipokwenda nchini Oman kucheza soka la kulipwa na tofauti na wengine ambao huingia mikataba na vilabu, yeye alipelekwa moja kwa moja katika kambi ya Timu ya Taifa ya Oman.
“Nilifikia kambi ya Timu ya Taifa ya Oman iliyokuwa Matra Hotel na Mei kulikuwa na mashindano ya nchi za Mataifa ya Asia na yale ya Mataifa ya Afrika,” alisema na kuongeza kwamba nchi hiyo ilikuwa mwenyeji wa michuano hiyo.
Mchezaji huyo alisema, Oman haikuwa na wachezaji wanaocheza soka la ushindani ambalo lingewawezesha kufika mbali katika michuano hiyo, hali ambayo iliwafanya watafute nguvu kazi kutoka nje ya mipaka yao ndipo walipomchukua yeye.
Wakati alisema alipewa mkataba wa miezi mitatu na akiwa na timu hiyo alikutana pia na wachezaji wengine wawili kutoka Kenya ambao ni Issa Ali na Jamal Stith na waliiwezesha timu hiyo kushika nafasi ya nne katika michuano hiyo.
“Miaka yote walikuwa wakishika mkia katika timu nane ambazo zilikuwa zinashiriki na Iraq mwaka huo waliibuka mabingwa wa michuano hiyo,” aliyataja mataifa mengine yaliyoshiriki michuano hiyo kuwa ni pamoja na Kuwait, Israel, Indonesia, Malaysia, Vietnam, Saud Arabia na Japan.
Mchezaji huyo alisema ingawaje walishika nafasi ya nne lakini furaha ya raia wa nchi hiyo ilikuwa kubwa sana, wachezaji walitunukiwa zawadi za kutosha, wakatembea vifua mbele katika mitaa ya nchi hiyo wakiitwa kila jina zuri kutokana na hatua waliyofikia.
Mchakato Fanja
Baada ya kumalizika kwa michuano hiyo, viongozi wa Chama cha Soka Oman (AFC), walimueleza wazi kuwa mkataba wake umeisha na kama kuna timu inamhitaji anaweza kuzungumza nao na ndipo walipojitokeza viongozi wa soka wa Klabu ya Fanja.
Klabu hiyo ilimtangazia dau na marupurupu mengine ili ajiunge nao, hivyo alikubaliana nao na akalazimika kurudi Zanzibar kusubiri kukamilishwa kwa taratibu na alirejea katika timu yake ya Small Simba ambayo ilikuwa inaendelea na Ligi ya Soka Visiwani humo na baadaye ile ya Muungano.
Wakati aliwataja wachezaji wengine wa Kitanzania walijiunga na Fanja mwaka uliofuata na vilabu walivyotokea katika mabano kuwa ni pamoja na Hilaly Hemed (Coastal Union), Ahmed Amasha (Yanga), Zahoro Salum (Malindi), Ramadhani Lenny (Simba), Madaraka Suleiman (Simba) na Hassan Hinai (Kenya).
“Wote tuliendelea kuichezea pia Timu ya Taifa ya Oman kasoro Lenny na Madaraka,” alisema.
Wakati alisema beki wa zamani wa Yanga na Timu ya Taifa ya Tanzania, Amasha bado anaishi Oman akilitumikia jeshi la nchi hiyo huku akiifundisha Timu ya Soka ya Al-Naseeb ya nchini humo.
Akiwa na Fanja na mseto wa wachezaji hao kutoka Tanzania, Fanja ilitisha na kuchua kombe la klabu bingwa kwa nchi za Ghuba baada ya kuifunga Timu ya Taifa ya Bahrain.
“Kwanza tulitwaa ubingwa wa Oman, kisha kombe la vilabu vya nchi za Ghuba,” alisema Wakati na kuongeza kwamba mchezo wa fainali ulikuwa na msisimko wa namna yake kwani hadi kipindi cha pili wapinzani wao walikuwa mbele kwa mabao 3-2.
Mchezaji huyo alisema walilazimika kufanya kazi ya ziada kusaka ushindi, mabao mawili aliyoyafungwa moja katika dakika ya 10 na lingine dakika tano baadaye yaliufanya mchezo huo uishe kwa sare ya mabao 5-5 na kufikia hatua ya kupigiana penalti zilizowapa ushindi.
Atungiwa sheria Zanzibar
Mara bada ya ubingwa alirudi nyumbani na kuendelea kuichezea timu yake ya Small Simba lakini katika hali isiyo ya kawaida, Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA) mwaka 1987 kilitunga sheria ya kupiga marufuku mchezaji anayecheza soka la kulipwa nje kucheza ligi ya nyumbani.
“Ni kama sheria hiyo nilitungiwa mimi maana ndiye mchezaji pekee wa Zanzibar niliyekuwa nikicheza soka la kulipwa nje na ligi ya ndani,” alisema.
Katika hali hiyo ilimbidi kila alipokuwa akirudi nyumbani akawa anasaidiana na Abdulghan Msoma kuifundisha Small Simba.
Soka la sasa
Mkongwe huyo ambaye aliichezea Timu ya Taifa ya Zanzibar kwa miaka 10 na kuchaguliwa Taifa Stars mwaka 1985, alisema vijana wa sasa hawana nguvu wala uwezo wa kutosha wa umiliki wa mpira hali ambayo inachangiwa na ukosefu wa mazoezi na kutojituma kwao.
“Ni vigumu kufanikiwa kupitia mazoezi ya mwalimu pekee, ni lazima uwe na muda wa kutosha wa mazoezi yako ili kujiongezea nguvu, stamina na uwezo wa kumiliki mpira,” alisema.
Thamani ya mchezaji
Wakati alisema kwamba kuna mchezaji visiwani humo aliomba kusajiliwa na klabu mojawapo na alipoulizwa kiasi cha fedha anachohitaji alisema apewe 100,000 lakini wakati wa mazoezi ya kumjaribu mchezaji huyo, hakuwa hata na thamani ya shilingi 50,000.
Wakati anabainisha kuwa, imefika sehemu wachezaji hawajui hata thamani zao na hata viwango vyao hawavitambui na mbaya zaidi wale wanaopata nafasi wakiwa na uwezo wakisifiwa kidogo wanabweteka.
Itaendelea Jumanne ijayo, Mwandishi anapatikana katika +2557826468