NGAO YA JAMII 2026: Macho yote KMC Dabi ya Kariakoo
Muktasari:
- Ngao ya jamii kwa wanawake inazikutanisha timu nne zilizomaliza nafasi nne za juu zilizomaliza Ligi Kuu msimu uliopita zikiwemo dabi mbili zenye msisimko wa pekee; dabi ya kati ya timu za jeshi kati ya JKT Queens iliyomaliza nafasi ya pili dhidi ya Mashujaa Queens (nafasi ya nne), na Dabi ya Karikoo kati ya mabingwa watetezi Simba Queens dhidi ya Yanga Princess iliyomaliza nafasi ya tatu.
PAZIA la msimu mpya wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara (WPL) linafunguliwa rasmi leo, Septemba 30, kwenye Uwanja wa KMC, Mwenge jijini Dar es Salaam, zikipigwa mechi mbili za nusu fainali ya Ngao ya Jamii.
Ngao ya jamii kwa wanawake inazikutanisha timu nne zilizomaliza nafasi nne za juu zilizomaliza Ligi Kuu msimu uliopita zikiwemo dabi mbili zenye msisimko wa pekee; dabi ya kati ya timu za jeshi kati ya JKT Queens iliyomaliza nafasi ya pili dhidi ya Mashujaa Queens (nafasi ya nne), na Dabi ya Karikoo kati ya mabingwa watetezi Simba Queens dhidi ya Yanga Princess iliyomaliza nafasi ya tatu.
Macho na masikio ya mashabiki wengi wa soka yataelekezwa kwenye Dabi ya Kariakoo. Hapa ndipo miamba miwili ya soka la wanawake itakapochuana kusaka tiketi ya fainali.
REKODI ZA TIMU
Simba Queens wanaingia kwenye mchezo huu wakiwa na jeuri ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu na ubora wa kimbinu ambao wameujenga kwa miaka kadhaa sasa.
Wekundu wa Msimbazi wamekuwa na utulivu mkubwa kwenye mechi kubwa, wakijivunia rekodi nzuri ya ushindi dhidi ya watani wao wa jadi katika mechi walizokutana.
Tangu mashindano hayo yaanzishwe mwaka 2023 ni Simba iliyobeba taji hilo mara moja (2023) na JKT Queens iliyonyakua miaka miwili mfululizo (2024/2025).
Simba na Yanga zimekutana mara tatu, mechi mbili zikitoka sare na moja Simba ikishinda. Utulivu wao wa kiutawala na uzoefu wa kikosi chao katika kucheza mechi za presha kubwa umewafanya waingie uwanjani wakijiamini.
Yanga wanaingia kwenye dabi hii wakiwa na shauku kubwa ya kufuta unyonge na kuonyesha mageuzi makubwa yaliyofanyika kwenye usajili wa msimu huu.
MAENEO YATAKAYOAMUA
Eneo ambalo linatarajiwa kuamua mchezo huu ni katikati ya uwanja. Hapa ndipo mbinu, ubunifu, na nguvu zitakapokutana.
Simba Queens wanajivunia safu ya kiungo ambayo haijabadilika sana, jambo linalowapa faida kubwa ya kuelewana (chemistry). Uwepo wa wachezaji waliozoea ligi na wenye uzoefu wa miaka mingi kama Elizabeth Mkuki, Vivian Corazone, Elizabeth Wambui na Brice Zanga unawapa utulivu mkubwa wa kumiliki mpira, kupunguza presha na kupanga mashambulizi kuanzia nyuma.
Corazone na Zanga wanajulikana kwa uwezo wao wa kukabili na kuzuia mashambulizi ya wapinzani, huku Mkuki na Wambui wakitoa ubunifu na kasi ya kulisha safu ya ushambuliaji.
Kwa upande wa Yanga Princess, eneo hilo limefanyiwa maboresho makubwa na linatabiriwa kuleta ushindani wa hali ya juu. Wanajivunia uzoefu wa Agnes Pallangyo, ambaye anaijua vizuri ligi ya ndani na ana uwezo wa kusoma mchezo na kutuliza presha.
Kando yake, Yanga wameongeza nguvu ya kwa kumsajili Joanita Nabirye kutoka Uganda pamoja na Tems Getanga aliyetokea klabu bingwa ya CBE ya Ethiopia. Mchanganyiko huu wa nguvu, uzoefu wa kimataifa, na ufundi unawafanya Yanga kuwa hatari kwenye eneo la kiungo, kwani wana uwezo wa kushindana kimwili na kuzuia Simba wasimiliki mpira kwa urahisi.
SAFU ZAO ZA USHAMBULIAJI
Ushindani mwingine mkali unatarajiwa kuonekana kwenye maeneo ya ushambuliaji na timu zote mbili zimefanya maboresho makubwa.
Simba inangia kwenye mechi hiyo ikiwakosa washambuliaji wake, Jentrix Shikangwa aliyetimkia FC Masar ya Misri, nyota huyo alikuwa mwiba mkali kwa Yanga kwa kasi yake na ubora wake wa kupachika mabao.
Hata hivyo, imesajili mbadala wake Senaf Semise kutoka CBE ya Ethiopia ubora aliouonyesha ubora kwenye mashindano ya CECAFA mwaka 2024 alikuwa mfungaji bora wa michuano hiyo akifunga mabao sita.
Sambamba naye, usajili wa Mary Siyame aliyetokea Fountain Gate Princess na Rida Kusamfulla kutoka Cameroon umeongeza nguvu eneo la mbele la timu hiyo inayotafuta taji lake la pili.
Kwa upande wa Yanga Sandrine Mutuyimana, aliyesajiliwa kutoka Inyemera WFC ya Rwanda, anatarajiwa kuwa mwiba mchungu kwa mabeki wa Simba kutokana na uwezo wake wa kutafuta nafasi, alisajiliwa kuziba nafasi ya Jeaninne Mukandayisenga aliyetimkia China.
Mbali na Mutuyimana ambaye alimaliza na mabao 10 msimu uliopita, Yanga pia wana nyota wengine Rehema Ramadhan (kutoka Fountain Gate Princess) na winga machachari Winifrida Charles, ambao kwa pamoja wanaunda safu ya ushambuliaji yenye kasi na uwezo wa kushambulia kwa kushitukiza.
NINI KITAAMUA MCHEZO?
Nusu fainali hii itaamuliwa na maeneo matatu ikiwemo utulivu wa kiungo. Timu itakayotawala eneo la katikati na kuzuia pasi za mwisho za mpinzani itakuwa na nafasi kubwa ya kushinda.
Kutumia Nafasi kwa kuwa hii ni mechi ya mtoano na ya mapema msimu, makosa machache ya safu za ulinzi yanaweza kuwa na faida kwa washambuliaji wapya wa pande zote mbili.
Mbinu za makocha wawili zitaamua kama ni Mussa Hassan ‘Mgosi’ wa Simba Queens au Edna Lema wa Yanga Princess aambaye mwenye mbinu bora ataondoka na ushindi.
WASIKIE HAWA
Koca wa Simba, Mgosi anasema “Tunajua ni dabi ina heshima yake hivyo tunaingia tukiwaheshimu wapinzani wetu lakini tunaamini tutafanya vizuri kwa sababu tulijiandaa vizuri.”
Nahodha wa Mashujaa, Fatuma Mustafa anasema “Tumejiandaa vizuri kucheza na JKT ambayo ni timu ngumu tupo tayari kushinda na tunaahidi tutapambana kuhakikisha mambo yanakuwa mazuri.”