Aisha Masaka, Clara Luvanga warejea Twiga Stars
Muktasari:
- Katika kikosi hicho, Shime amewajumuisha Aisha Masaka na Clara Luvanga, sambamba na nyota wengine wanaocheza soka ndani na nje ya Tanzania.
KOCHA wa Timu ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars, Bakari Shime, ameita kikosi cha wachezaji 23 kitakachoingia kambini Oktoba 1, 2026 kwa ajili ya maandalizi ya michezo miwili ya kufuzu Olimpiki dhidi ya Botswana.
Katika kikosi hicho, Shime amewajumuisha Aisha Masaka na Clara Luvanga, sambamba na nyota wengine wanaocheza soka ndani na nje ya Tanzania.
Masaka anarejea kwenye kikosi hicho baada ya kukosekana kwa muda mrefu kutokana na changamoto ya majeraha, hali iliyomfanya kukaa nje kwa sehemu kubwa ya msimu uliopita.
Nyota huyo wa Brighton & Hove Albion, alipata jeraha la bega Novemba 2024 katika mchezo wa Ligi Kuu Wanawake England dhidi ya Arsenal, lililomfanya akae nje ya uwanja kwa miezi kadhaa akipitia matibabu na kurejea taratibu mazoezini.
Uwepo wake sasa unaongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji ya Twiga Stars, hasa kutokana na uzoefu aliojijengea akiwa kwenye soka la Ulaya na England.
Mbali na Masaka, Shime amemrudisha Luvanga ambaye kwa sasa anaichezea Washington Spirit ya Marekani baada ya kuondoka Al Nassr ya Saudi Arabia. Luvanga anaingia kwenye kikosi akiwa na kumbukumbu nzuri ya msimu uliopita baada ya kufunga mabao 24 kwenye Ligi Kuu ya Wanawake Saudi Arabia, kabla ya kuhamia Marekani. Mshambuliaji huyo aliitwa katika kikosi cha WAFCON Juni 18, 2026 lakini hakucheza, kabla ya sasa kuitwa tena.
Kikosi hicho kina wachezaji saba kutoka JKT Queens ikiwa ndiyo timu iliyotoa idadi kubwa, ikifuatiwa na Simba Queens yenye sita. Fountain Gate Princess na Yanga Princess zimeingiza mchezaji mmoja mmoja.
Wachezaji walioitwa kwenye kikosi hicho ni Diana Mnally (Yanga Princess), Nusra Hamis (Fountain Gate), Najiath Abbas, Anastazia Katunzi, Ester Maseke, Winfrida Castor, Bahati Steven, Asha Rashid na Elizabeth Chenge (wote JKT Queens).
Pia wapo Janeth Shija, Vaileth Nicholaus, Fatuma Issa, Elizabeth Joseph, Mary Siyame, Aisha Mnunka (wote Simba Queens).
Kwa upande wa wachezaji wanaocheza nje ya Tanzania, kikosi hicho kina Noela Luhala wa MFA Žalgiris ya Lithuania, Diana Msewa (Trabzonspor, Uturuki), Hasnath Ubamba (Madrid CFF, Hispania), Opah Clement (Alula Club, Saudi Arabia), Enekia Lunyamila (Gallos Femenil, Mexico), Julittha Singano (Al Nassr, Asaudi Arabia), Masaka na Luvanga.
Twiga Stars inatarajia kuanza maandalizi Oktoba 1, ikiwa na jukumu la kujiandaa kwa michezo miwili dhidi ya Botswana, huku mchezo wa kwanza ukipangwa kuchezwa ugenini Oktoba 9, 2026 na wa marudiano nchini Tanzania Oktoba 13, 2026.