Nchimbi; mambo matano tangu afunge bao Ligi Kuu
KAMA hujui ni kwamba leo Jumatatu ni siku 380 kamili tangu mshambuliaji wa Yanga na Taifa Stars, Ditram Nchimbi alipofunga mabao yake kwenye mechi za Ligi Kuu Bara.
Ndio, kwani mara ya mwisho kwa Nchimbi kutupia nyavuni ilikuwa Februari 29, 2020 na mshambuliaji hiyo aliyesajiliwa Yanga Desemba 19, 2019 akiwa kambi ya timu ya taifa, Taifa Stars iliyokuwa nchini Uganda ikishiriki mashindano ya Chalenji amekuwa na ukame usiomithilika.
Turejee nyuma kidogo, kiwango alichokionyesha katika mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Yanga na Polisi Tanzania uliofanyika Oktoba 3, 2019 ndio kiliwavutia viongozi wa Jangwani kuamua kumsajili Nchimbi baada ya kuwazidi akili Polisi iliyokuwa ikimtumia kwa mkopo kutoka Azam FC.
Katika mchezo huo Nchimbi buana, alipiga hat trick na kuisumbua sana ngome ya Yanga kwani ni mmoja wa wachezaji wapambanaji uwanjani na wanaotumia nguvu kubwa na mashabiki waliamini akiungana na wakali wa Jangwani anaweza kuwa moto zaidi ya ule aliokuwa nao Polisi.
Ndani ya kipindi hicho cha mwaka mmoja ambacho Nchimbi hajafunga bao ndani ya Yanga kuna mambo zaidi ya 100 ambayo yametokea duniani - waliokuwa wajawazito wamejifungua hadi watoto waliowazaa wamesherehekea bethidei zao za kutimiza mwaka mmoja, watu mashuhuri kadhaa wamefariki dunia, mtaani kwako umeshuhudia matukio kadhaa ndani ya muda huo na katika soka la kimataifa mengi yametokea; na kadhalika na kadhalika. Lakini Mwanaspoti leo linakuletea baadhi tu ya matukio yaliyotokea tangu Nchimbi alipofunga bao lake la mwisho akiwa na jezi za Yanga.
Janga la Corona
Wakati Nchimbi anasajiliwa Yanga ndio Corona nayo iliingia Tanzania baada ya mtanzania mmoja mwanamke mwenye umri wa miaka 46 kupima na kubainika kuwa na virusi vya ugonjwa huo baada ya kutua kwenye uwanja wa ndege wa Kilimanjaro akitokea Ubelgiji mabapo pia alipita Sweden na Dernmark.
Kutokana na ugonjwa huo kungia nchini, Machi 17 ilimlazimu Waziri Mkuu wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Kassim Majaliwa kuzungumza na vyombo vya habari na kutangaza kusimamisha shughuli mbalimbali za kijamii ili kuepusha maambukizi zaidi.
Waziri mkuu Majaliwa alisema”Serikali imechukua hatua kadhaa za awali ili kuweza kukabiliana na tatizo hili ikiwemo kuzuia mikusanyiko yote mikubwa ya ndani na nje isiyokuwa ya lazima ili kuzuia maambukizi.
“Tumefunga shule zote za awali, msingi sekondari na zitafungwa kwa mda wa siku 30 kuanzia leo Machi 17 na tumeisitisha michezo yote inayokusanya makundi yote kama vile Ligi Kuu Bara, na michezo ya shule za msingi (umitashumta), michezo ya shule za sekondari (Umiseta) pamoja na ile ya mashirika ya uma inayopangwa kwenye ratiba kila mwaka,” alisema Waziri mkuu.
Baada ya taarifa hiyo,Machi 18 Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilisimamisha ligi zake zote ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali huku pia ikivunja kambi ya timu ya taifa, Taifa Stars ambayo ilikuwa inajiandaa na fainali za Mataifa ya Afrika (CHAN) zilizopangwa kuanza Aprili 4 hadi 25, mwaka huu nchini Cameroon.
Baada ya miezi miwili, Mei 17 Rais wa Jamhuri ya ,Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli akiwa kwenye ibada katika kanisa la kiinjili la Kilutheri wilayani Chato Geita alisema wagonjwa walipungua sana hadi kufikia kipindi hicho hivyo alifikiria kufungua vyuo ili wanafunzi waendelee kusoma na kuruhusu michezo kwani ni sehemu ya burudani kwa watanzania na ndipo Juni 14 mwaka jana Ligi Kuu bara msimu wa 2019/2020 iliendelea tena mpaka ilipofikia tamati Julai 26.
Yanga yatimua, yaleta makocha
Licha ya kudumu ndani Yanga kwa maka mmoja akipita chini ya makocha watatu tofauti lakini bado jambo hilo halijaweza kumbeba Nchimbi na kufunga.
Makocha hao wote watatu kwa sasa wametimuliwa na klabu hiyo na kumuacha Nchimbi akiendelea kupambana na hali yake katika kutafuta bao litakalompa morali ya kufunga mengine zaidi.
Nchimbi alianza kuwa chini ya kocha Luc Eymael ambaye alitua ndani ya timu hiyo Januari mwaka jana na alidumu kwa miezi saba tu kabla ya kutimuliwa Julai 27 kutokana na kutoa kauli za kibaguzi dhidi ya mashabiki na viongozi wa klabu hiyo pamoja na TFF.
Baada ya kuondoka Eymael, Yanga ikamleta kocha mwingine mserbia, Zlatko Krmpotic Agosti mwaka jana ambaye licha ya kudumu kwa mwezi mmoja tu ndani ya klabu hiyo alishindwa kuwa msaada kwa Nchimbi kufunga bao hadi alipoondoka Oktoba.
Ukame wa mabao kwa Nchimbi uliendelea hata pale Yanga ilipomuajiri mrundi Cedric Kaze ambaye licha ya kwamba alikuwa akimpa nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza mara nyingi lakini mchezaji huyo alishindwa kutikisa nyavu za wapinzani wake.
Kaze alitua ndani ya timu hiyo Oktoba 15 mwaka jana lakini hata hivyo amedumu kwa miezi mitano tu kabla ya Machi 7 mwaka huu kutupiwa virago kutokaa na mwenendo mbaya wa Yanga kwenye ligi.
Simba yakomba mataji, yatinga makundi CAF
Nchimbi alitua Yanga katka usajili wa dirisha dogo msimu uliopita lakini mpaka ligi inamalizika Julai mwaka jana na Simba ikatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la ASFC na kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya CAF, wakati mchezaji huyo alikuwa hajatikisa nyavu za timu pinzani.
Wakati Nchimbi akipambana na hali yake Jangwani, Simba ilifanya vyema kwenye mechi zake za awali na kufanikiwa kutinga makundi na kwa sasa ikiongoza kundi lake lenye vigogo Al Ahly ya Misri, AS Vita ya DR Congo na Al Merrikh ya Sudan na huenda Mnyama akatinga robo fainali, wakati Nchimbi akiendeleza gundu lake la kutotupia kambani.
Namungo kimataifa
Sio Simba tu, wakati Nchimbi akiendelea kuyumba uwanjani bila kufunga bao, Wauaji wa Kusini, Namungo imewasapraizi Watanzania kwa kutinga kwenye michuano ya kimataifa baada ya kufika fainali za ASFC na kufungwa na Simba na kukata tiketi kwa vile Wekundu pia walibebea taji la VPL.
Dodoma Jiji, Gwambina, Ihefu zapandA TPL
Wakati Nchimbi akiendelea kuhaha kusaka mabao, Dodoma Jiji, Ihefu na Gwambina zimeshuhudiwa zikipanda daraja na zinaendelea kukinukisha kwenye Ligi Kuu Bara, ilihali Mbeya City iliyokuwa ikielekea kushuka daraja nayo ikisalimika.