Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NBC yamwaga mikopo ya mabasi klabu Ligi Kuu

Mkurugenzi wa Fedha wa benki ya NBC  Waziri Barnabas akizungumza na washiriki wa Mkutano Mkuu wa kawaida wa 17 wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) uliofanyika jijini Mwanza hii leo.

Mwanza. Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ambaye ni mdhamini mkuu wa Ligi Kuu ya Soka ya Tanzania Bara (NBC Premiere League) imesisitiza kuhusu dhamira yake ya kuboresha zaidi ligi hiyo kwa kuendelea kuziwezesha timu zinazoshiriki ligi hiyo ili ziweze kujenga uwezo wa kujitegemea.

Dhamira hiyo imesisitizwa na Mkurugenzi wa Fedha wa benki hiyo, Waziri Barnabas mapema jana wakati akizungumza na washiriki wa mkutano mkuu wa kawaida wa 17 wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) uliofanyika jijini Mwanza.

“Kimsingi ni kwamba sisi kama wadhamini wa ligi hii tunajivunia sana kuona ligi yenye ushindani na viwango bora vya kiuchezaji vinavyoendelea kuonekana kwenye ligi hii. Hii inatokana na timu zinazoshiriki ligi hii kuweza kusajili na wachezaji wazuri kutoka ndani na nje ya nchi sambamba na kuweza kuwahudumia vema wachezaji hao ikiwemo kuwapatia maslahi yao.’’ alisema

Waziri alisema mbali na udhamini wa ligi hiyo benki hiyo imebuni mikakati mbalimbali inayolenga kufanikisha dhamira hiyo muhimu ikiwemo mikopo ya mabasi kwa klabu mbalimbali zinazoshiriki ligi hiyo ili kurahisisha usafiri.

“Ligi hii inahusisha suala zima la usafiri kwa klabu husika na wakati mwingine timu zinasafiri kwa umbali mrefu sana na hivyo kusababisha uchovu kwa wachezaji. Upatikanaji wa mabasi mazuri ya kisasa utasaidia kupunguza uchovu kwa wacheza ili waweze kuleta ushindani unaohitajika wakiwa viwanjani. Tupo kwenye hatua nzuri na hivi karibuni baadhi ya timu zitapatiwa mabasi yao,’’ alisema.

Waziri alitaja huduma nyingine kuwa ni pamoja na utoaji wa bima kwa wachezaji, benchi za ufundi na familia za wachezaji wote wa ligi hii ya NBC Premier League.

“Tunaamini kuwa Bima hizi ambazo tunazitoa kupitia kampuni washirika za Britam na Sanlam, zimekuwa chachu kubwa kwa kuwaondolea wachezaji hofu za kucheza kwa woga wakihofia kupata majeraha yanayoweza kuathiri ajira zao. Hili limechochea sana wachezaji wetu kuonyesha viwango vyao.’’ Alisema.

Aidha Bw Waziri aliwaomba wadau hao wamichezo zikiwemo klabu, viongozi wa mchezo huo na wachezaji mmoja mmoja kuhakikisha wanachangamkia fursa ya kuwekeza kwenye hati Fungani ya NBC Twiga Bond ili waweze kunufaika na faida mbalimbali zitokazo na Hati fungani hiyo.

“Kiasi cha chini cha ununuzi wa hati fungani hiyo ni Sh500, 000. Kupitia uwekezaji huu wahusika wataweza kupata riba kubwa ya 10% kwa mwaka, inayolipwa nusu mwaka katika kipindi chote cha miaka mitano hadi Novemba 2027. Kiwango cha riba kinacholipwa hakina punguzo la kodi. Hivyo nawakaribisha sana wadau wa michezo’’ alisema