NBC Dodoma Marathon yazinduliwa, kusaidia matibabu saratani ya shingo ya kizazi
Muktasari:
- Zaidi ya wakimbiaji 6,000 kutoka nchi mbalimbali wanatarajia kushiriki mbio za NBC Dodoma Marathon Julai 23, 2023 zenye lengo la kukusanya fedha za kugharamia matibabu ya saratani ya shingo ya kizazi na kuchangia kutoa ufadhili wa elimu kwa wanafunzi wanaosomea taaluma ya ukunga ili kuboresha afya ya mama wa mtoto
Dodoma. Benki ya NBC imetangaza kufanyika mbio kubwa za NBC Dodoma Marathon Julai 23, 2023 mkoani Dodoma lengo kuu ikiwa ni kukusanya fedha za kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi na kuchangia kutoa ufadhili wa elimu kwa wanafunzi wanaosomea taaluma ya ukunga ili kuboresha afya ya mama wa mtoto.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne, Mei 23, 2023, Mkurugenzi wa Fedha wa Benki hiyo, Waziri Barnabas amesema; “Kupitia mbio hizi za NBC Dodoma Marathon, tunalenga kuchangia katika kuboresha afya ya uzazi kupitia sapoti kwenye mapambano dhidi ya kansa ya shingo ya kizazi kwa wanawake na pia kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa taaluma ya ukunga nchini,”
“Tunaamini kupitia shindano hili tuweza kuisaidia jamii yetu kupambana na changamoto hizi. Kupitia ufadhili wa wanafunzi wa elimu ya ukunga itasaidia kukabiliana na upungufu wa wataalamu hao na hivyo kupunguza vifo vya kina mama wakati wa uzazi,” alisema
Alisema vilevile wanaendelea na msaada katika mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi ambapo mpaka sasa wameshakusanya zaidi ya Sh500 milioni zilizosaidia kufikia upimaji wa saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake zaidi ya 23,500 na matibabu kwa zaidi ya wanawake 1,300.
Kuhusu mchango wa NBC kwenye sekta ya michezo nchini, Barnabas alisema; ”NBC inatambua na kuthamini sana umuhimu wa michezo katika ujenzi wa taifa hususan katika kutoa ajira na kuongeza pato la taifa.”
“Hivyo basi, tumeendelea kuwekeza katika michezo ikiwemo udhamini wetu mkubwa wa Ligi Kuu ya soka Tanzania yaani NBC Premier League ambayo imekuwa na matokeo chanya sana kwa taifa letu. Tunajivunia kuwa wadau wakubwa wa michezo nchini,” amesema
Aidha, Mkurugenzi huyo alitumia fursa hiyo kuwapongeza na kuwashukuru taasisi ya ORCI (Ocean Road Cancer Institute) na Benjamin William Mkapa kuwa wabunifu na kwa huduma wanazotoa ili kusaidia jamii kuimarisha afya ya mama na mtoto.
Vilevile aliwashukuru wadau wa mashirika na makampuni mbali mbali kama Sanlam, Jubilee General Insurance, Garda World, Cheknocrafts, Icea Lions Insurance, Metropolitan Life Insurance, Strategies Insurance, Hans Paul, SBC- Pepsi, na Aramex kwa udhamini wao ili kufanikisha mbio hizi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ORCI), Julius Mwaiselage alisema taasisi hiyo inafurahia kujumuika tena katika mbio hizi jijini Dodoma baada ya mafanikio awali.
“Dhamira yetu ni kuendelea kutoa elimu zaidi ya saratani ya shingo ya kizazi ili kuimarisha afya ya mama na mtoto nchini. Saratani ya Shingo ya Kizazi, ndiyo inayoongoza kwa kusababisha vifo vingi zaidi vinavyohusiana na saratani kwa wanawake nchini Tanzania,” alisema
Alisema jambo la kutia moyo ni kwamba saratani hii inaweza kuzuilika na kutibiwa iwapo itagundulika mapema. Na kwa kuimarisha afya ya mama na mtoto tunajenga taifa lenye uwezo zaidi. Ni jukumu letu kwa pamoja kuunga mkono serikali yetu katika kuongeza uelewa na kuchangia uimarishaji wa afya za mama na watoto kulinda kizazi kijacho.
Kwa Upande wake Mkurugenzi wa programu kutoka Benjamin Mkapa Foundation alisema; “Nina furaha kujumuika na NBC katika mbio hizi kwani fedha zitakazo patikana katika mbio hizi zitasaidia kusomesha wakunga zaidi na kuboresha huduma ya afya kwa mama na mtoto na hivyo kujenga taifa lenye afya bora, tatizo hili ni kubwa na uhaba wa wataalamu hawa ni mkubwa hivyo tunawasihi watanzania kujumuika katika mbio hizi kuchangia upatikanaji wa fedha ili tuweze kukabiliana na uhaba huu kwa pamoja” alisema