Nasma Manduta kutimkia Uturuki
Muktasari:
- Kama dili hilo litakamilika Manduta ataungana na Mtanzania mwenzake Diana Msewa anayekipiga Trabzonspor ya nchi hiyo ambaye huu ni msimu wake wa tatu sasa.
KIUNGO wa Tanzania, Nasma Manduta yuko mbioni kujiunga na Antalya Spor ya Ligi ya Wanawake Uturuki kwa msimu mmoja akitokea Ceasiaa Queens ya Iringa.
Kama dili hilo litakamilika Manduta ataungana na Mtanzania mwenzake Diana Msewa anayekipiga Trabzonspor ya nchi hiyo ambaye huu ni msimu wake wa tatu sasa.
Kwa mujibu wa chanzo cha ndani kutoka kwa mchezaji mpango wa ulikuwa kiungo huyo kucheza Lithuania ambako ndiko alikuwa na ofa kubwa, lakini mchakato wa kukamilisha uhamisho huo umeonekana kuwa mrefu.
Baada ya kumaliza mkataba wa mwaka mmoja sasa ndipo wasimamizi wake wataanza mchakato wa kumpeleka Lithunia ambako na Uturuki ni rahisi zaidi ukilinganisha na Tanzania.
“Nasma ataenda Uturuki kwanza kucheza msimu mmoja, kisha baada ya hapo ataelekea Lithuania kwa sababu mchakato wa uhamisho ni mrefu kutoka Tanzania, Tunaamini mambo yatakaa sawa hivi karibuni,” kilisema chanzo hiko.
Manduta, ambaye aliwahi kuitumikia Yanga Princess, Gets Program na Baobab Queens ya Dodoma kupelekwa Uturuki pia ni moja ya sababu ya kumuongezea uzoefu na kukuza karia yake.
Mbali na hilo pia kiungo huyo aliitwa kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Futsal kilichocheza mashi ndano ya Kombe la Dunia la Futsal.