Namna nyingine ya kumtumia Ndayiragije
Muktasari:
Mimi ni shabiki wa Etienne Ndayiragije na ninaamini kwamba kuwa kwake na Kilimanjaro Stars au Zanzibar Heroes kwenye mashindano ya Chalenji kungempa fursa nyingine adhimu ya kuwajua na kuwafundisha wachezaji wake kuliko kumwacha akae afuatilie mashindano kama washabiki.
KOCHA Msaidizi wa Taifa Stars, Juma Mgunda, amekabidhiwa mikoba ya kuinoa Kilimanjaro Stars katika michuano ya Chalenji inayoanza wikiendi hii nchini Uganda. Kwa upande wa Zanzibar, wao wamempa jukumu hilo Hemed Morocco.
Huu ni uamuzi unaotokana na busara ya muda mrefu kwenye kutofautisha majukumu ya Kocha Mkuu wa Taifa Stars katika nchi ambayo ni Muungano wa nchi mbili. Hii si mara ya kwanza kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kufanya uamuzi wa namna hii.
Ni uamuzi ambao, kwa maoni yangu, ni wa kisiasa zaidi kuliko kimichezo. Sijawahi kuona mantiki yake kimichezo kwa sababu hakuna sababu ya kumnyima Kocha Mkuu nafasi ya kukaa na timu ambayo asilimia 80 ya wachezaji wanaotumika ndiyo wale anaowafundisha kwenye timu ya taifa.
Mimi ni shabiki wa Etienne Ndayiragije na ninaamini kwamba kuwa kwake na Kilimanjaro Stars au Zanzibar Heroes kwenye mashindano ya Chalenji kungempa fursa nyingine adhimu ya kuwajua na kuwafundisha wachezaji wake kuliko kumwacha akae afuatilie mashindano kama washabiki.
Nimewahi kufanya kazi kwenye vilabu vya soka na ninajua walau kidogo kwamba, kukaa na kuishi na wachezaji ni kitu tofauti na kujifunza kuhusu wao kwa kuwatazama wakiwa uwanjani. Nimewahi kushuhudia wachezaji wa aina tofauti sana.
Wapo wachezaji ambao ni wazuri sana mazoezini, lakini kwenye mechi hawawezi kuonyesha walichonacho. Kuna wengine kwenye mechi ni wazuri sana lakini mazoezini unaweza kudhani ni magoigoi hivi. Hii ni tabia ya wachezaji iliyotamalaki karibu dunia nzima.
Mimi ninadhani kwamba kama Tanzania imeajiri kocha mtaalamu kutoka nje, ni afadhali kwa mwalimu huyo kutumika kwa kupokezana mwaka hadi mwaka. Kwamba Chalenji ya mwaka huu akiwa Stars, mwakani apewe Heroes. Ni muhimu kuangalia zaidi namna ya kuwatumia walimu wetu kuliko kutafuta namna ya kuonekana tunafanya jambo sahihi kisiasa.
Uganda ina mwalimu mmoja. Kenya ina mwalimu mmoja na karibu kila timu ina mwalimu mmoja. Tuchukulie mfano wa Uganda ambayo imeamua kutumia wachezaji wake wa ndani pekee kwenye mashindani haya. Maana yake ni kwamba kocha wao sasa atakuwa na nafasi ya kuwafahamu wachezaji wengi zaidi wa taifa lake kuliko kama angeng’ang’ania nyota walio nje.
Kuna kitu kinaniambia kwamba hatujawahi kufanya kazi kubwa ya kusaka na kutumia vipaji vilivyoko Zanzibar. Karibu kila mwaka au miaka miwili, kuna mchezaji hutokea visiwani ambaye anakuja kujulikana vizuri akicheza kwenye Mapinduzi Cup au akiwa mchezaji wa Simba, Yanga au Azam.
Ningetamani siku moja kocha wa Stars apewe mikoba ya kufundisha Zanzibar Heroes kwenye mashindano kama haya ya Chalenji. Aende na kuonana na wachezaji wa Pemba na Unguja. Afahamu tabia zao, uchezaji wao na mambo yao. Ataifahamu Zanzibar na Wazanzibari.
Akirudi kwenye majukumu ya Stars na kukutana na Wazanzibari kambini, atakuwa anawafahamu vizuri zaidi na kuelewa ni mambo gani yanawafanya wawe kwenye kiwango cha juu na yepi huwa yanawashusha morali.
Mwaka unaofuata anafundisha Kilimanjaro na unaofuata anarudi tena Zanzibar. Kama akifukuzwa, anayeletwa mwingine anakwenda kufundisha kwa kuangalia aliyepita alikuwa kwenye nchi ipi mwaka uliopita.
Kwa mtazamo wangu, hii ndiyo namna ya kufaidika zaidi na utaalamu uliopo kuliko hii ya sasa ya kuogopa upande mmoja unanufaika zaidi na makocha wa kigeni kuliko mwingine. Na ukiniuliza zaidi, nitakwambia ninachoamini kitaimarisha zaidi Muungano na kutufanya wamoja zaidi kuliko kinachofanyika sasa.
Bunju, Mwanahiba na MwanaSpoti
Kama kuna tukio ambalo linahusishwa zaidi na wakati wangu nilipokuwa Katibu Mkuu wa klabu ya Simba basi ni tukio la kuanza kwa maandalizi ya Uwanja wa Bunju ambao wanachama wa Simba watakwenda kuona maendeleo yake wikiendi hii.
Nilifanya kampeni kubwa kupitia vyombo vya habari kuhamasisha washabiki na wanachama wa Simba wafahamu kwamba, kuna eneo lao lililoko Bunju ambalo lilinunuliwa wakati wa uongozi wa akina Hassan Dalali na Mwina Kaduguda.
Alichofanya Ismail Aden Rage wakati wa uongozi wake na akina Geofrey Nyange, ilikuwa ni kulipa gharama zilizotakiwa kulipwa kwa serikali. Mimi kazi yangu ilikuwa ni kupiga debe tu. Nilitamani sana Simba iwe na uwanja wake yenyewe na pia matokeo hayakuwa mazuri uwanjani na nilitaka wanachama wa klabu wawe angalau na jambo la kujivunia wanapobishana na wenzao vijiweni.
Hata hivyo, kuna watu muhimu ambao Simba SC inatakiwa itafute namna ya kuwaenzi kwa mchango wao. Wa kwanza ni mwandishi wa gazeti hili, Mwanahiba Richard, ambaye alilifanya jambo la uwanja wa Simba kuwa kama ajenda yake binafsi na gazeti lake.
Alikuwa akiandika mara kwa mara, kwa kwenda mwenyewe katika eneo husika na kuibua mambo tofauti kwa kufanya mahojiano na watu mbalimbali. Ilikuwa wazi kwamba Mwanahiba hataacha kuandika hadi pale uwanja huo ukamilike. Nadhani kuna haja ya kufanya kitu kwa ajili yake katika wakati mwafaka. Anaweza kutajwa kwa kupewa tuzo binafsi kama ishara ya shukrani au namna nyingine ambayo itawafanya waandishi wengine kuona kwamba, wanaweza pia kuamua kuandika mambo mazuri ambayo hayako viwanjani lakini yana maslahi makubwa kwa maendeleo ya michezo hapa nchini.
Katika hili, ni lazima niseme kwa kwa heshima na taadhima, navua kofia kwa Mwanahiba na MwanaSpoti.