Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mzuka wa Niyonzima wambeba Jangwani

Muktasari:

  • Unajua kwanini? Niyonzima anajua soka bwana, misimu yake karibu sita aliyocheza Yanga iliwapa burudani mashabiki hao, ndio maana baadhi yao kwa hasira walifikia hatua ya kuchoma jezi yenye namba nane kwa kuona Mnyarwanda huyo kawasaliti.

KIPINDI dirisha kubwa la usajili likifanyika mwanzoni mwa msimu huu, mashabiki wengi wa Yanga walionekana kuchanganyikiwa walipojihakikishia kuwa, kiungo wao fundi, Haruna Niyonzima ametua Msimbazi.

Unajua kwanini? Niyonzima anajua soka bwana, misimu yake karibu sita aliyocheza Yanga iliwapa burudani mashabiki hao, ndio maana baadhi yao kwa hasira walifikia hatua ya kuchoma jezi yenye namba nane kwa kuona Mnyarwanda huyo kawasaliti.

Walisahau kuwa, soka ni ajira ya kiungo huyo na ilikuwa lazima siku moja ataondoka Jangwani kama alivyokuja bila kutarajiwa mwanzoni mwa miaka ya 2010.

Mashabiki wengi walionekana kupaniki, lakini mabosi wao walituliza kichwa na kufanya usajili kadhaa kwa kuwapelekea Papy Kabamba Tshishimbi na Ibrahim Ajibu kabla ya kumpandisha dogo fulani mtamu hivi, Maka Edward.

Maka alipandishwa sambamba na wenzake kadhaa akiwamo mawinga Said Mussa, Yusuph Mhilu, lakini cha ajabu wote waliikata jezi namba nane ya Niyonzima na kujua mikononi mwa Maka ambaye anaonekana kufuata nyayo za mkali huyo.

Nyota ya Maka ilianza kung’ara katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi ya mwaka huu kwa kucheza kwa kiwango cha juu na baadaye kuliamsha dude katika baadhi ya mechi za Ligi Kuu kabla ya kuitwa timu ya taifa ya Vijana U-20.

ALIKOANZIA SOKA

Maka anasema soka alilianza kulicheza katika akademi za mtaani kabla hajaonekana na kikosi cha Yanga chini ya miaka 20.

“Nilianza kucheza soka akademi ya Archipelago ipo Aiport Dar es Salaam, lakini baadaye nikaenda Bom Bom SC, nakumbuka tulicheza mechi ya kirafiki na Yanga B, ndipo waliniona kisha wakaongea na kocha wangu Hamidu Kibonge wakanichukua.”

Anaongeza kwamba alivyoambiwa kama anahitajika na kikosi hicho aliamini kabisa kwamba ameshaanza kuingia katika ramani ya soka inayoeleweka.

“Baada ya kucheza sana katika akademi niliona sasa umefika muda wa kucheza katika timu yoyote ya vijana katika ligi kuu, hivyo walivyokuja Yanga, sikuwa na hiyana badala yake niliona fursa.”

YANGA YAMBADILISHA

Baada ya kutoka katika akademi na kupata nafasi katika kikosi cha vijana mpaka timu ya wakubwa, Maka anasema kitendo hicho kimembadilisha soka lake kiujumla.

“Mabadiliko yapo mengi katika soka langu, sasa hivi nina nguvu ya kupambana kwa dakika zote, lakini hata akili ya soka imeongezeka kwavile nimekutana na mbinu mpya.”

Maka anadai katika kikosi hicho inabidi uwe na uvumilivu kwa kila hali kwa sababu ni timu yenye mashabiki wengi.

UGUMU WA NAMBA

Kama ilivyo katika vikosi vyote ugumu wa namba ni changamoto, basi hata kwa Yanga hali ndio hiyo na imemkuta kiungo huyu ambaye alikuwa akipata nafasi katika kikosi kilichocheza Mapinduzi Cup.

“Naichukulia kama changamoto tu kwangu kwani, bado mdogo na nina muda mwingi wa kucheza nikijitunza, naamini mwalimu anajua muda sahihi ni upi wa kunitumia kwa sababu bado najua kuna vitu bado sijakamilika na ndio ananijenga.”

Hata hivyo anaongeza kwamba hatoacha kujituma na kulishawishi benchi la ufundi ili kuweza kupata nafasi.

JEZI YA NIYO MZUKA MTUPU

Iko hivi. Baada ya Niyonzima kuondoka jezi yake namba 8, ilikuwa haivaliwi na mtu yeyote katika kikosi cha Yanga.

Lakini dogo huyu baada ya kupandishwa alifumba macho na kuivaa, huku wenzake wakiwa hawamuamini.

“Nadhani watu walianza kuniona nayo nikiwa Mapinduzi, lakini wakati napewa ile jezi wengi walikuwa wanahoji kama nitaiweza? Lakini huwezi amini kila ninapoivaa ndiyo inanipa nguvu ya kufanya vizuri ili niweze kuaminiwa na jezi hii,” anasema.

NGORONGORO HEROES

Baada ya kuonekana katika kikosi cha Yanga, benchi la ufundi la timu ya vijana Taifa ‘Ngorongoro Heroes’, ilimuita lakini hajafanikiwa kucheza mechi yoyote katika mechi mbili walizocheza hivi sasa.

“Ni jambo zuri kuwa katika kikosi cha vijana, wapo wengi wanaotamani kuwepo pale hivyo sitorudi nyuma zaidi ya kufanya vizuri ili nipate nafasi katika timu ya wakubwa.’’

“Sijafanikiwa kucheza lakini naamini nitacheza kwa sababu uwezo ninao, kitu kinachohitajika ni uvumilivu lakini nikipewa nafasi nifanye vizuri na kulishawishi benchi la ufundi.”

MALENGO YAKE

Kila mchezaji huwa na ndoto yake ya kutaka kufika mbali katika soka, basi hata kwa kiungo huyu pia hali ni ile ile.

“Mimi ni kijana mdogo ambaye nahitaji kufika mbali, natakiwa nifanye vizuri hapa nilipo ili niweze kuonekana, lakini hivi sasa nipo katika njia sahihi ya kufika mbali ikiwezakana hata kupata klabu nje ya nchi,” anasema.