Mzize alivyohitimisha siku 489 Yanga
Muktasari:
Katika mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, Mzize alifunga bao moja dakika ya 76 likiwa la kwanza kwake msimu wa 2026-2027 la Ligi Kuu Bara tangu mara ya mwisho alipofunga dhidi ya Simba, Juni 25, 2025.
MSHAMBULIAJI wa Yanga, Clement Mzize amehitimisha siku 489 za kukaa bila kufunga bao la Ligi Kuu Bara, ambazo ni sawa na mwaka mmoja na siku 124 baada ya juzi kuifungia timu hiyo katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mashujaa FC.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, Mzize alifunga bao moja dakika ya 76 likiwa la kwanza kwake msimu wa 2026-2027 la Ligi Kuu Bara tangu mara ya mwisho alipofunga dhidi ya Simba, Juni 25, 2025.
Mzize aliyeingia dakika ya 70 akichukua nafasi ya Juma Issa Abushiri alifunga bao hilo la ushindi dakika ya 76 na moja likifungwa na Peter Shalulile dakika ya 21, huku la upande wa Mashujaa likifungwa na Crispin Ngushi dakika ya nane.
Kufunga kwa mshambuliaji huyo bao hilo, kumemfanya kuhitimisha ukame wa mwaka mmoja na siku 124 ambazo ni sawa na siku 489 tangu mara ya mwisho alipoifungia Yanga katika ushindi wa kikosi hicho wa mabao 2-0 dhidi ya Simba, Juni 25, 2025.
Katika mechi hiyo Mzize alifunga bao dakika ya 86 na lingine likifungwa na Pacome Zouzoua kwa penalti dakika ya 66 na kuipa Yanga ubingwa wa 31 wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-2025 tangu mwaka 1965 baada ya kufikisha pointi 82.
Mzize aliyeanzia timu ya vijana ya Yanga kabla ya kupandishwa kikosi cha wakubwa huu ni msimu wake wa tano katika Ligi Kuu Bara, ambapo msimu wa kwanza wa 2022-2023 alifunga mabao matano, huku msimu wa 2023-2024 akimaliza na mabao sita. Msimu wa 2024-2025, ndio bora zaidi kwa Mzize baada ya kufunga mabao 14, akishika nafasi ya pili kwa nyota waliofunga mengi nyuma ya aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa Simba, Jean Charles Ahoua aliyekuwa mfungaji bora kwa kufunga mabao 16.
Baada ya kuonyesha kiwango cha kuvutia msimu wa 2025-2026 ulikuwa mgumu kwa mshambuliaji huyo baada ya kuandamwa zaidi na majeraha yaliyomfanya asifunge bao lolote, japo msimu wa 2026-2027 amerudi upya na kufungua ukurasa wake wa mabao.
Nyota huyo kwa sasa anatoa ushindani mkubwa wa eneo la ushambuliaji na wachezaji wenzake wakiongozwa na Peter Shalulile anayeongoza kikosini akiwa na mabao matano ya Ligi Kuu na Cheikh Ibrahima Toure ambaye ameshaifungia timu hiyo bao moja.
Mzize aliyechanguliwa mchezaji bora wa mechi ya juzi dhidi ya Mashujaa FC alinukuliwa akisema bao alilolifungwa limemuongezea morali ya kuzidi kupambana zaidi kikosini humo, baada ya kukosekana kwa muda mrefu uwanjani.