Mzimu wa penalti waitesa Namungo
Muktasari:
- Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi, Namungo ilikosa penalti dakika ya 15, iliyopigwa na Awesu Awesu na kupanguliwa na kipa, Frank Faustine, kisha Hashim Manyanya akaifungia bao dakika ya 25.
MZIMU wa kukosa penalti kwa wachezaji wa Namungo katika Ligi Kuu Bara, umeendelea kukitesa kikosi hicho, baada ya kushuhudia Agosti 18, 2026, ikikosa tena, licha ya kushinda bao 1-0 dhidi ya Geita Gold.
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi, Namungo ilikosa penalti dakika ya 15, iliyopigwa na Awesu Awesu na kupanguliwa na kipa, Frank Faustine, kisha Hashim Manyanya akaifungia bao dakika ya 25.
Tangu msimu wa 2025-2026, hadi huu wa sasa 2026-2027, Namungo ni timu iliyopiga penalti nyingi zaidi ambazo ni nane, ikiwa ni idadi sawa na Singida Black Stars, ikifuatiwa na mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Yanga na Simba zilizopiga saba kila moja.
Katika penalti hizo nane ambazo Namungo FC imepiga huku saba zikiwa za msimu wa 2025-2026 na moja ya msimu wa 2026-2027, wachezaji wa kikosi hicho wamefunga tatu kati ya hizo, huku tano wakikosa na kuendelea kushindwa kutumia nafasi vizuri.
Penalti hizo tatu zilizofungwa ambazo ni za msimu wa 2025-2026, waliofunga ni Cyprian Kipenye aliyepo hadi sasa, Fabrice Ngoy ambaye anacheza Geita Gold na Heritier Makambo aliyeondoka ndani ya kikosi hicho.
Katika penalti tano zilizokoswa, nne ni za msimu wa 2025-2026 na waliokosa ni Fabrice Ngoy aliyekosa mbili, Lucas Kikoti na Cyprian Kipenye wakikosa moja moja kila mmoja, huku msimu wa 2026-2027, Awesu Awesu akianza kwa kukosa.
Awesu aliyejiunga na Simba Julai 16, 2024, baada ya kuachana na KMC FC, alishindwa kupenya katika kikosi cha kwanza na dirisha dogo la Januari 2026, aliichezea Kenya Police FC ya Kenya kwa mkopo na mkataba wake ulipoisha akatua Namungo.
Akizungumzia suala hilo, Kocha Mkuu wa Namungo, Juma Mgunda alisema licha ya kiungo huyo wa zamani wa Kagera Sugar, Azam na Mwadui kukosa penalti hiyo, lakini ataendelea kupiga kwa sababu amekuwa akifanyia kazi tangu akiwa mazoezini.
“Ile penalti hatujampa kwa bahati mbaya, amekuwa akifanya vizuri mazoezini ndio maana alichukua jukumu lile, kwangu bado ataendelea kupiga kwa sababu mchezaji yeyote anaweza akakosa pia, niseme wazi ni chaguo letu la kwanza,” alisema Mgunda.