Mpole atoa ahadi nzito mashujaa
Muktasari:
- Mpole ambaye Januari 2026 alitua Tanzania Prisons, katika msimu wa 2025-2026 alifunga mabao saba kwenye Ligi Kuu Bara, hivyo anahitaji kuvuka idadi hiyo ili kuisaidia Mashujaa kufanya vizuri. Kumbuka Mashujaa ilimaliza msimu na mabao 15.
MSHAMBULIAJI George Mpole aliyetua Mashujaa kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea Tanzania Prisons, amesema anajipanga kuhakikisha huduma yake inakuwa na manufaa ingawa jambo la msingi zaidi anatamani kumaliza na mabao zaidi ya yale aliyoyafunga msimu uliopita.
Mpole ambaye Januari 2026 alitua Tanzania Prisons, katika msimu wa 2025-2026 alifunga mabao saba kwenye Ligi Kuu Bara, hivyo anahitaji kuvuka idadi hiyo ili kuisaidia Mashujaa kufanya vizuri. Kumbuka Mashujaa ilimaliza msimu na mabao 15.
“Nilipigiwa simu na viongozi muda mfupi kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili, hivyo sikusita kuja kusaini mkataba ingawa nilikuwa na ofa tofauti ikiwepo za nje, ila niliona ni muda sahihi wa kuichezea Mashujaa,” alisema Mpole na kuongeza;
“Natamani kufunga mabao zaidi ya saba ambayo nilimaliza nayo msimu uliopita ingawa natambua kuna ushindani mkubwa, hilo nachukulia kama chachu ya kupambana zaidi.”
Msimu wa 2022-2023 akiwa na Geita Gold, Mpole aliibuka kinara wa ufungaji Ligi Kuu Bara akifunga mabao 17 sawa na aliyomaliza nayo aliyekuwa mshambuliaji wa Singida Black Stars, Mossi Ndumumwe aliyekuwa mfungaji bora 2025-2026.
Mpole baada ya kufanya vizuri 2022-2023, alitimkia FC Lupopo ya DR Congo, lakini maisha hayakuwa mazuri, akarejea nchini kuichezea Pamba Jiji, ndipo akaibukia Tanzania Prisons na sasa Mashujaa.