Mzimu mwingine kwa Pamba, Kagera
Muktasari:
- Hii ni baada ya timu hizo pekee Ligi Kuu ukanda huo kumaliza dakika 540 zikikusanya pointi mbili kwa Kagera Sugar na moja kwa Pamba Jiji na kuweka presha ndani na nje ya uwanja juu ya hatma ya miamba hao.
WAKATI Ligi Kuu ikifikia raundi ya saba kwa baadhi ya timu, mzimu mpya umeonekana kuziandama Pamba Jiji na Kagera Sugar, huku wadau na mashabiki wakihofia Kanda ya Ziwa kukosa uhondo wa michuano hiyo msimu ujao.
Hii ni baada ya timu hizo pekee Ligi Kuu ukanda huo kumaliza dakika 540 zikikusanya pointi mbili kwa Kagera Sugar na moja kwa Pamba Jiji na kuweka presha ndani na nje ya uwanja juu ya hatma ya miamba hao.
Hadi sasa timu hizo ndizo zinaburuza mkia katika nafasi mbili za mwisho, ambapo Kagera Sugar yuko nafasi ya 15 kwa pointi mbili, ilhali Pamba Jiji wakiwa nafasi ya 16 kwa pointi moja.
Kagera Sugar waliorejea Ligi Kuu msimu huu baada ya kudumu Championship msimu mmoja, hawajawa na matokeo mazuri huku Pamba Jiji waliokuwa na kiwango bora msimu uliopita, hali imeonekana kuwa tofauti.
Katika historia Kanda ya Ziwa iliwahi kutamba katika medani za soka, ikiwa na idadi kubwa ya timu za Ligi Kuu, ni Kagera Sugar, Toto Africans, Mwadui, Stand United, Biashara United na Rhino Rangers. Nyingine zilizoibuka na kisha kupotea ni Mbao FC, Alliance FC, Gwambina, Pamba Jiji, Geita Gold na Tabora United (kwa sasa TRA United) na kwa sasa hofu imeanza kutanda kuweza kuzipoteza zote.
Kwa sasa Kanda hiyo ina timu tatu Ligi Kuu, ambazo ni Pamba Jiji waliowahi kutwaa ubingwa wa Kombe la Muungano mwaka 1999, Kagera Sugar na Geita Gold ambayo ndio inapumua katika nafasi ya tisa kwa pointi saba.
Mdau wa soka ambaye aliwahi kuwa mhasibu wa Toto Africans, Aboubakari Seif, amesema licha ya Pamba Jiji kuwa na kikosi bora haijawa na mwanzo mzuri na huwa inawakuta wengi ambao hawana maandalizi mazuri na tatizo ni upepo kutokuwa mzuri kwao.
“Kushuka daraja si ajabu lazima wajipange, kumbuka timu ina maingizo mapya haihitaji kuungaunga, lazima wajipange vinginevyo tunaweza kusikia au kuona mengine, ligi ni ngumu kila mtu ajitume kwa nafasi yake,” amesema.
Kwa upande wake Respicius John amesema kutokana na matokeo yasiyoridhisha kwa Kagera Sugar, uongozi na wamiliki wa timu hiyo wanapaswa na kukaa na benchi la ufundi na wachezaji kufanya tathimini kujua tatizo.