Mgunda aanza kuona mwanga Simba
Muktasari:
- Mgunda amesema mechi za CAF zina ushindani wa hali ya juu, hivyo kupewa nafasi ya kucheza na kocha Barker kunaendelea kumjengea kujiamini na kuzidi kujituma, ili huduma yake iendelee kuwa muhimu Simba.
KITENDO cha Kocha wa Simba, Steve Barker kumpa nafasi ya kucheza mshambuliaji wa timu hiyo, Ismail Mgunda mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mighty Wanderers, kimechukuliwa kwa uzito na mchezaji huyo, akiamini ni mwanzo mzuri wa kufanya vizuri zaidi.
Mgunda amesema mechi za CAF zina ushindani wa hali ya juu, hivyo kupewa nafasi ya kucheza na kocha Barker kunaendelea kumjengea kujiamini na kuzidi kujituma, ili huduma yake iendelee kuwa muhimu Simba.
“Ilikuwa mechi nzuri kwani tumepata ushindi wa kishindo, lakini binafsi kupata nafasi ni faraja kubwa, morali ya kupambana kuamini mechi zinazokuja nitafanya vizuri zaidi,” amesema Mgunda na kuongeza;
“Haijalishi nimecheza dakika ngapi, jambo la msingi ni kupata muda wa kucheza na kuonyesha kiwango ambacho kitaendelea kumshawishi kocha aendelee kunipanga tena.”
Katika mechi hiyo ambayo Simba ilishinda kwa mabao 6-1 baada ya kutoka Elie Mpanzu, aliingia Mgunda ambapo alitoa pasi ya bao dakika ya 88 lililofungwa na Keletso Makgalwa.
Data zake kabla ya kujiunga na Simba msimu huu akitokea Mashujaa: 2023/24 alifunga mabao sita akiwa na Singida BS 2024/25 alienda kucheza ligi ya Congo katika klabu ya AS Vita na 2025/26 alimaliza na mabao mawili.