Yanga yaongeza nguvu benchi la ufundi
Muktasari:
- Ekotto aliyewahi kufanya kazi akiwa na timu za KMC FC na Mlandege FC ya Zanzibar, amejiunga na kikosi hicho ili kwenda kuongeza nguvu zaidi katika benchi la ufundi la kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Mkuu, Manqoba Mngqithi.
KLABU ya Yanga, imeendelea kufanya maboresho ya benchi la ufundi la timu hiyo baada ya kumuongeza ndani ya kikosi hicho kocha mwingine wa viungo, Abdulwahid Abdallah ‘Ekotto’, akienda kushirikiana kwa ukaribu na Tshephang Mokaila ‘Chyna’.
Ekotto aliyewahi kufanya kazi akiwa na timu za KMC FC na Mlandege FC ya Zanzibar, amejiunga na kikosi hicho ili kwenda kuongeza nguvu zaidi katika benchi la ufundi la kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Mkuu, Manqoba Mngqithi.
Kocha huyo anaungana na Chyna raia wa Botswana ambaye amefikisha msimu wake wa pili na kikosi hicho tangu ajiunge nacho akitokea AmaZulu FC ya Afrika Kusini, akiendelea kuboresha zaidi utimamu wa wachezaji.
Ongezeko la Ekotto linaifanya Yanga kuwa na benchi la ufundi la wataalamu saba wa kiufundi, likiongezwa na Kocha Mkuu, Manqoba Mngqithi aliyejiunga na timu hiyo Julai 10, 2026, baada ya kuachana na Golden Arrows FC ya Afrika Kusini.
Kwa upande wa Kocha Msaidizi ni Simo Dladla aliyetokea Amazulu FC ya kwao Afrika Kusini, Kocha wa Makipa Mnigeria, Greg Etaif na Kocha wa Viungo, Tshephang Mokaila ‘Chyna’ anayeungana kwa sasa kikosini humo na Ekotto ili kuongeza pia nguvu.
Wengine wanaounda benchi la ufundi ni Kocha wa Mipira ya Kutenga (set-piece), Kagisho Dikgacoi na Mtathmini Mchezo (Video Analyst), Yardaan Valodia ambao wote wamejiunga na kikosi hicho wakitokea Golden Arrows FC ya kwao Afrika Kusini.
Kujiunga kwa Ekotto anaenda kuongeza nguvu kwa kushirikiana na Chyna ambaye tayari ana uzoefu na kikosi hicho ambacho anakitumikia kwa msimu wa pili sasa, kwa lengo la kutengeneza utimamu wa wachezaji hasa kutokana na mashindano mengi.
Yanga imeanza kampeni ya kutetea taji lake la 31 wa Ligi Kuu Bara.