Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwana FA anogesha Exim Bima Festival

Naibu Waziri Wa Utamaduni, Sanaa Na Michezo, Hamis Mwinjuma (Mwana FA), mwishoni mwa wiki alipamba  msimu wa kwanza wa Tamasha la Bima Festival lililoratibiwa na benki ya Exim Tanzania huku akitoa wito kwa kampuni za bima na taasisi za fedha nchini  kuongeza ufadhili wao kwenye sekta ya michezo  ili kuchochea zaidi kasi ya ukuaji wa sekta hiyo inayokua kwa kasi.

Mwinjuma aliziomba taasisi hizo kubuni huduma mbalimbali zinazolenga kuwasaidia wadau wa sekta ya michezo na burudani nchini.

Katika tamasha hilo lililoratibiwa  kwa ushirikiano na wadau mbalimbali wa sekta ya bima nchini zikiwemo kampuni za Alliance life Assurance Limited, Alliance Insurance Corporation Limited, Jubilee Allianz General Insurance Company Limited, Strategis Insurance Company Limited, The Heritage Insurance Tanzania na kampuni wateja wa benki hiyo ikiwemo kampuni ya bidhaa za plastic ya CELLO pamoja na kampuni ya uchimbaji madini ya Taifa Mining, ilishuhudiwa timu ya mpira wa miguu ya Exim ikiibuka mshindi wa jumla kwenye mashindano ya mpira wa miguu yaliyohusisha wadau wote.

Akizungumza wakati akizindua tamasha hilo Mwinjuma pamoja na kuwapongeza wadau hao kwa kuandaa tukio hilo lililotoa fursa ya  kufurahia pamoja,  kubadilishana mawazo na kujengeana ufahamu zaidi kuhusu huduma zao,  aliwasihi wajitokeze zaidi kuunga mkono shughuli mbalimbali zinazofanywa na wadau wa michezo na burudani nchini kwa kudhamini shughuli zao mbalimbali na kuwatumia kwenye hamasa za kibiashara yakiwemo matangazo.

“Mchango wenu unaweza kutafsiriwa katika maeneo mengi ya kimichezo lakini msisitizo wangu nauweka zaidi katika udhamini wa matukio mbalimbali ya michezo hususani katika uibuaji wa vipaji na kusaidia vilabu mbalimbali vinavyoshiriki ligi mbalimbali hapa nchini ikiwemo ligi Kuu. Zaidi pia niwaombe muendelee kubuni huduma za bima na huduma za kifedha mahususi kwa wanamichezo na wasanii ili muwasaidie kulinda afya na kazi zao na zaidi kuwajenga kiuchumi.’’ alisema.

Pia Mwinjuma aliipongeza benki hiyo kwa jitihada zake za kukuza michezo hapa nchini kupitia msaada wa vifaa vya michezo inavyotoa kwa shule za msingi na sekondari katika mikoa mbalimbali hapa nchini.

‘Mmeonyesha dhamira na nia njema ya kuinua vipaji vya vijana na kuwezesha maendeleo ya michezo nchini. Tunatambua mchango wenu mkubwa katika kuendeleza michezo na tunawashukuru kwa kuwa wabia wetu katika kufanikisha malengo yetu ya kitaifa katika sekta hii,” alisema huku pia akionesha matumaini makubwa kuwa tamasha la Exim Bima Festival litakuwa na mafanikio makubwa na litaleta matunda yaliyotarajiwa.


Awali, akizungumza kwa niaba ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim, Mkuu wa Idara ya Uwekezaji Kimkakati na Matawi ya Nje wa benki hiyo Sumit Shekhar, alisema  kupitia tamasha hilo litakalokuwa likifanyika kila mwaka, benki hiyo imejipanga kutumia vema fursa  ya michezo na burudani kuboresha mahusiano yake na wadau wake mbalimbali wakiwemo wateja, wadau wa bima, wafanyakazi, mamlaka mbalimbali zinazosimamia sekta ya bima na benki pamoja na serikali.

“Tukiwa kama wadau muhimu wa sekta ya fedha na bima nchini kupitia huduma yetu ya Bima ijulikanayo kama ‘Bima tu Malipo Tuachie’ tumejipanga kuhakikisha tunalitumia vema tamasha hili kama mkakati muhimu wa kuboresha mahusiano baina yetu na wadau wetu tukiamini mahusiano ndio nguzo ya kwanza kwenye biashara yoyote na tamasha la Exim Bima Festival linakuja kama namna bora ya kutusaidia kufanikisha hilo,’’ alisema Shekhar.

Akizungumzia ushindi wa jumla katika mashindano ya mpira wa miguu baina ya wadau hao, mfungaji bora katika mashindano hayo Calvin Kilua kutoka timu ya benki ya Exim alisema siri ya mafanikio ni timu yake kujiandaa vema kwa ajili mashindano hayo sambamba na kutafsiri vema maelekezo ya kocha wa  timu hiyo ambae ni Meneja Rasilimali Watu, Mikidadi Ngoma.

“Baada ya mafanikio haya tunaamini kwamba tamasha lijalo litahusisha timu nyingi zaidi na ushindani utaongezeka. Hivyo tutaendelea kujiweka sawa kwa mazoezi zaidi kwa kuwa mazoezi pia ni afya na ukizungumzia afya ni moja ya agenda ya msingi kwenye huduma zetu za bima,’’ alisema Stanley Kafu, Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa benki ya Exim.