Mwana FA ahitimisha Stan Cup Manyara
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Hamis Mwinyijuma maarufu kama MwanaFA (katikati) aliwakabidhi kombe mabingwa wa michuano ya soka ya Stan CUP Manyara Sugar iliyofanyika kata ya Magugu wilayani Babati mkoani Manyara. Picha na Joseph Lyimo
Muktasari:
- Michuano ya Stan Cup imeshirikisha timu 18 za soka kata ya Magugu wilayani Babati mkoani Manyara na bingwa wake akajinyakulia kombe na fedha taslimu Sh3.3 millioni
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinyijuma maarufu kama Mwana FA, amehitimisha michuano ya Diwani wa Magugu wilayani Babati, Stan Cup kwa timu ya Manyara Sugar kuibuka washindi.
Mwana FA amekuwa mgeni rasmi katika michuano hiyo iliyoshirikisha timu 18 huku Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Regina Ndege akiwa mgeni mwalikwa.
Akizungumza kwenye fainali ya michuano hiyo iliyofanyika uwanja wa Magugu, Mwana FA amesema michuano hiyo imeonyesha ukubwa wake kwenye ngazi ya kata.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Ndege akiikagua timu ya Magugu Rangers kwenye fainali ya michuano ya Stan CUP iliyofanyika kata ya Magugu wilayani Babati mkoani Manyara. Picha na Joseph Lyimo
Ametoa pongezi kwa waandaji wa mashindano hayo ya Stan Cup kwani yamekuwa na hamasa kubwa na zawadi kubwa katika ngazi ya kata.
Hata hivyo, ameeleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele kuwainua vijana kwa namna alivyowekeza kwenye michezo hivyo viongozi na Watanzania kwa ujumla wamuunge mkono.
"Rais Samia amewekeza katika michezo hasa mpira wa miguu nchini na mwakani 2027 tutakuwa wenyeji pacha, Tanzania tukishirikiana na Kenya na Uganda, kwenye michuano ya Kombe la AFCON," amesema.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Hamis Mwinyijuma maarufu kama MwanaFA (kulia) ambaye ni mgeni rasmi wa michuano ya Stan CUP alikaribishwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Regina Ndege kwenye michuano hiyo ya soka iliyofanyika kata ya Magugu wilayani Babati mkoani Manyara. Picha na Joseph Lyimo
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Ndege ambaye pia ni mbunge wa viti maalum mkoa wa Manyara, amempongeza diwani huyo kwa kuandaa michuano hiyo.
"Hongera sana diwani wa Magugu kwa kuandaa Stan Cup kwani vijana na wana Magugu kwa ujumla wamehamasika kuhudhuria na kuonyesha kuwa michezo ni furaha, amani na upendo," amesema.
Diwani wa kata ya Magugu, Stanley Dismas amemshukuru Naibu Waziri Mwana FA kwa kuwa mgeni rasmi na Naibu Waziri, Regina kwa kumshika mkono katika kuendesha michuano hiyo.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Ndege (watisa kushoto) akiwa na mabingwa wa Stan CUP timu ya Manyara Sugar kwenye fainali iliyofanyika kata ya Magugu wilayani Babati mkoani Manyara. Picha na Joseph Lyimo
Katika michuano hiyo iliyoshirikisha timu 18 za eneo hilo, Manyara Sugar ilitwaa ubingwa wa Stan Cup kwa kuichapa Magugu Rangers mabao 2-0 na kujinyakulia kombe na fedha taslimu Sh3.3 milioni.