Mwalwisi akomaliza mafaza IAA SC
Muktasari:
- Timu ya IAA SC ya Arusha ilifuzu kucheza Ligi ya Championship kwa msimu wa 2026-2027, kupitia mechi ya 'Play-Off', baada ya kuitoa African Sports ya Tanga kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda nyumbani 2-1, kisha ugenini ikatoka sare ya bao 1-1.
KOCHA Mkuu wa IAA SC, Maka Mwalwisi amesema ugeni wa timu hiyo katika Ligi ya Championship, sio kigezo cha wao kufanya vibaya hadi sasa, isipokuwa bado hakuna muunganiko mzuri wa kiuchezaji, jambo analoendelea kulifanyia kazi kwa uharaka.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mwalwisi aliyejiunga na IAA SC ya jijini, Arusha akitokea Tabora United yenye maskani mjini, Tabora, amesema licha ya ugeni wao ila wachezaji wa kikosi hicho ni wazoefu, ingawa, wanakosa muunganiko wa kiuchezaji.
"Tuna wachezaji wengi wazoefu na Ligi ya Championship ila bado muunganiko wao kiuchezaji haujakaa vizuri, sio suala la wiki moja au mbili kwa sababu ni wapya na wanahitaji muda, tunaendelea kupambania jambo hilo haraka," amesema Mwalwisi.
Kocha huyo aliyezifundisha Ihefu kwa sasa Singida Black Stars na TMA FC iliyokuwa Arusha kisha kuhamishia makazi yake mjini, Iringa, amesema baada ya kumaliza raundi ya 15, ndiyo atakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kujua mwelekeo kijumla.
IAA SC inayoshiriki Ligi ya Championship msimu wa 2026-2027, kwa mara ya kwanza, kabla ya mechi ya jana Jumapili dhidi ya Mbuni FC ya Arusha pia, imeshinda miwili, ikitoka sare tano na kupoteza mitatu, ikishika nafasi ya 13 na pointi 11.
Timu ya IAA SC ya Arusha ilifuzu kucheza Ligi ya Championship kwa msimu wa 2026-2027, kupitia mechi ya 'Play-Off', baada ya kuitoa African Sports ya Tanga kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda nyumbani 2-1, kisha ugenini ikatoka sare ya bao 1-1.