Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwalimu atia timu Zanzibar, azuiwa kuzungumza

Muktasari:

  • Mwalimu amewasili Unguja mchana huu, akipokewa na Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji, huku mshambuliaji huyo akiwa amevalia mavazi rasmi ya klabu hiyo.

Mshambuliaji Selemani Mwalimu ‘Gomes’ amewasili Zanzibar tayari kuanza maisha mapya akiwa na Klabu ya Yanga.

Mwalimu amewasili Unguja mchana huu, akipokewa na Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji, huku mshambuliaji huyo akiwa amevalia mavazi rasmi ya klabu hiyo.

Mchezaji huyo amewasili sambamba na Meneja wa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, ambaye alikuwa naye tangu usiku wa kuamkia leo baada ya mshambuliaji huyo kukamilisha usajili wake na kusaini mkataba.

Hata hivyo, mara baada ya kuwasili, Arafat, Kamwe na Mwalimu hawakuwa tayari kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu usajili huo.

Mwalimu pekee alitoa kauli fupi akisema amezuiwa kuzungumza lolote kwa sasa.

Mshambuliaji huyo anatarajiwa kujiunga moja kwa moja na kikosi cha Yanga ambacho leo jioni kitafanya mazoezi ya mwisho kabla ya kukutana na Simba kesho katika mchezo wa Ngao ya Jamii utakaopigwa katika Uwanja wa New Amaan, Unguja, Zanzibar.

Yanga imemsajili Mwalimu kwa mkataba wa mkopo kutoka Wydad Casablanca ya Morocco baada ya kufanikiwa kufikia makubaliano.

Awali, Mwalimu alikuwa amekaribia kuongeza mkataba wake wa mkopo na Simba, lakini mabosi wa Wekundu hao walishindwa kukamilisha kwa wakati taratibu za malipo Wydad.

Hali hiyo iliipa Yanga nafasi ya kuingia kwenye mazungumzo na Wydad, huku mabosi wa klabu hiyo wakiwa tayari kukamilisha taratibu zote.

Mwalimu alikuwa kambini na Simba, Unguja hadi jana usiku, kabla ya kuondolewa na kurejeshwa Dar es Salaam kwa ndege maalumu.

Alikwenda Dar es Salaam kukamilisha usajili wake na kusaini mkataba mbele ya Rais wa Yanga, Hersi Said.

Hatua hiyo imekuja muda mfupi kabla ya mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, ambao sasa unaweza kuwa mwanzo wa Mwalimu kuanza  akiwa upande wa Yanga dhidi ya klabu yake ya zamani.