Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MultiChoice Tanzania yazindua kampeni ya Pata Zaidi, yapunguza bei za DStv

KIKOW Pict

MultiChoice Tanzania imezindua kampeni mpya ya “Pata Zaidi”, ikitangaza punguzo kubwa la bei za vifurushi vya DStv, kurahisisha huduma zake na kuongeza maudhui ya Kitanzania pamoja na vipindi vya michezo kwa lugha ya Kiswahili.

Maboresho hayo yaliyotangazwa jana, Novemba 3, 2026, yanahusisha kupunguza idadi ya vifurushi vya msingi kutoka sita hadi vinne, hatua inayolenga kurahisisha uchaguzi na kuwapa wateja huduma zinazoendana na mahitaji na uwezo wao wa kifedha.

Katika mabadiliko hayo, wapenzi wa michezo sasa wataweza kupata kifurushi kipya cha DStv Sports chenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA Champions League) kwa Sh50,000, kutoka Sh118,000 za awali.

Aidha, mashabiki wa Ligi Kuu England (EPL) sasa wataweza kufuatilia mashindano hayo kupitia kifurushi cha DStv Select kwa Sh25,000, badala ya Sh68,000 walizokuwa wakilipa kupitia kifurushi cha Compact.

Wateja wanaopendelea burudani za nyumbani, ikiwemo tamthilia, filamu na vichekesho, watanufaika na kifurushi cha DStv Starter kitakachogharimu Sh15,000 kutoka Sh27,500.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa MultiChoice Tanzania, Sophie Tchatchoua, alisema maboresho hayo yametokana na maoni ya wateja waliokuwa wakihitaji huduma nafuu, uchaguzi rahisi na maudhui yanayowakilisha maisha yao.

“Tumewasikiliza. Tumepunguza idadi ya vifurushi, tumeshusha bei na kuongeza maudhui yanayokidhi mahitaji ya wateja wetu. Tunataka wapate burudani zaidi, uchaguzi mpana na thamani bora kwa kila shilingi wanayotumia,” alisema.

Katika kukuza maudhui ya ndani, kampuni hiyo imetangaza tamthilia mpya ya KARATA, iliyozalishwa kikamilifu nchini na Watanzania, ikiwapa nafasi waigizaji na wabunifu wa ndani kuonesha vipaji vyao.

Pia imezindua SuperSport Swahili, chaneli itakayokuwa ikirusha matangazo na uchambuzi wa michezo ya kimataifa kwa Kiswahili.

Kwa upande wa maudhui ya watoto, MultiChoice imeongeza Ubongo Kids kwenye DStv, ikilenga kuunganisha elimu na burudani kwa kutumia Kiswahili.

Tchatchoua alisema kampeni ya Pata Zaidi ni sehemu ya mkakati wa kampuni hiyo wa kuweka wateja mbele, kukuza vipaji vya Kitanzania na kupanua upatikanaji wa burudani bora kwa gharama nafuu.

Aliongeza kuwa uwekezaji katika maudhui ya ndani utaendelea kuwa kipaumbele cha kampuni hiyo.