Mbeya City yavunja rekodi ikiinyoosha Singida Black Stars
Muktasari:
- Mbeya City imeshinda mchezo huo ikivunja uteja kwa SBS na kukinasua nafasi za chini na sasa inajiandaa na mchezo ujao dhidi ya Namungo kisha kuwapokea Yanga.
BAADA ya kukosa ushindi katika michezo sita mfululizo, hatimaye Mbeya City imefufuka ikiizamisha Singida Black Stars bao 1-0 na kupanda nafasi ya 11 kwa pointi 13.
Mbeya City ambayo msimu uliopita iliponea chupuchupu kushuka daraja kupitia play off, ilikuwa na mwanzo mzuri kabla ya mambo kuharibika na kukikuta katika presha ya kukosa ushindi.
Katika mechi sita za nyuma, timu ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya, ilipoteza nne na kupata sare mbili na kuwa nafasi tatu za chini na kuweka presha ndani na nje ya uwanja.
Ushindi huo ni wa kwanza kwa Mbeya City dhidi ya SBS katika historia kwani kwenye michezo minane waliyowahi kukutana, wamepoteza mitano na sare tatu na kuweka rekodi mpya.
Ikicheza leo kwa ubora licha ya mvua iliyonyesha na kufanya uwanja kutokuwa rafiki, ilionesha kiwango bora na kufanikiwa kupata bao la mapema dakika ya 22 kupitia kwa Rifati Hamis.
Singida Black Stars ambao wanajivunia kufuzu hatua ya makundi Kombe la shirikisho Afrika, walishuka uwanjani wakikumbuka ushindi wa mechi iliyopita dhidi ya Pamba Jiji ugenini na leo kujikuta wakiangusha pointi jijini Mbeya.
Licha ya timu zote kucheza kwa akili, nidhamu na kiwango bora, lakini wenyeji ndio waliweza kubaki na shangwe huku kipa wa Mbeya City raia wa Malawi, Frank Munthal ambaye ni mechi yake ya pili akianza na kipigo cha 4-0 dhidi ya Azam.