Vyakula vitano vinavyoweza kuboresha hali yako ya kihisia
Muktasari:
- Wataalamu wa afya ya akili na lishe wamekuwa wakieleza uhusiano uliopo kati ya chakula, ubongo na hisia. Utafiti uliochapishwa mwaka 2017 katika jarida la tiba la BMC ulionyesha kuwa kuboresha mfumo wa ulaji kunaweza kusaidia kupunguza dalili za sonona kwa baadhi ya watu. Hivi hapa ni vyakula vitano vinavyoweza kusaidia kuboresha hali yako ya kihisia.
Unapokuwa na mawazo mengi, msongo wa mawazo, kukosa furaha au kujikuta ukiwa na hasira bila sababu ya msingi, huenda ukahitaji kuangalia upya aina ya vyakula unavyokula.
Watu wengi wanapozungumzia afya ya kihisia huzingatia mapumziko na mazingira yanayowazunguka, lakini chakula pia kina mchango katika namna ubongo unavyofanya kazi na mwili unavyodhibiti hisia.
Wataalamu wa afya ya akili na lishe wamekuwa wakieleza uhusiano uliopo kati ya chakula, ubongo na hisia. Utafiti uliochapishwa mwaka 2017 katika jarida la tiba la BMC ulionyesha kuwa kuboresha mfumo wa ulaji kunaweza kusaidia kupunguza dalili za sonona kwa baadhi ya watu. Hivi hapa ni vyakula vitano vinavyoweza kusaidia kuboresha hali yako ya kihisia.
1. SAMAKI
Samaki kama dagaa, sangara, sato na samaki wenye mafuta mengi wana mafuta aina ya Omega-3 yanayosaidia utendaji wa kawaida wa ubongo. Mafuta haya ni muhimu katika afya ya mfumo wa fahamu na mawasiliano kati ya seli za ubongo.
Wataalamu wa lishe na afya ya akili wanaeleza kuwa mafuta haya yanaweza kuwa na mchango katika kupunguza baadhi ya dalili za msongo wa mawazo.
Utafiti uliofanyika mwaka 2019 na kujulikana kama HELFIMED pia ulionyesha kuwa mfumo bora wa ulaji uliojumuisha mafuta ya samaki ulihusishwa na kupungua kwa dalili za sonona kwa baadhi ya washiriki.
2. MBOGA ZA MAJANI
Mchicha, matembele, kisamvu na spinachi vina vitamini na madini mbalimbali yanayohitajika katika utendaji wa mwili na ubongo. Baadhi ya mboga hizi zina kirutubisho kinachoitwa folati, ambacho husaidia michakato mbalimbali ya mwili inayohusika na utengenezaji wa kemikali zinazowasilisha taarifa kwenye ubongo.
Wataalamu wa lishe wanasisitiza umuhimu wa kula mboga za majani mara kwa mara ili kukidhi mahitaji ya virutubisho muhimu. Utafiti wa mwaka 2017 pia ulihusisha ulaji wa mboga kama sehemu ya mabadiliko ya mfumo wa chakula yaliyosaidia kuboresha afya ya kihisia kwa baadhi ya washiriki.
3. KARANGA NA NJUGU
Karanga, korosho na njugu zina mafuta mazuri, protini na madini ya magnesiamu yanayosaidia utendaji wa kawaida wa mfumo wa fahamu. Magnesiamu ina nafasi katika michakato inayohusika na mawasiliano ya mishipa ya fahamu na utendaji wa misuli.
Kwa mujibu wa tafiti zinazohusu lishe na afya ya akili, ulaji wa karanga kama sehemu ya mfumo bora wa chakula umehusishwa na afya nzuri ya kihisia. Utafiti wa HELFIMED uliona pia uhusiano kati ya kuongezeka kwa ulaji wa karanga na kupungua kwa dalili za sonona.
4. NAFAKA ZISIZOKOBOLEWA
Vyakula kama ulezi, mtama, dona, shayiri na mchele wa kahawia vina nyuzinyuzi zinazosaidia mfumo wa chakula na kudhibiti mabadiliko ya sukari mwilini.
Sukari inapobadilika kwa kasi, baadhi ya watu wanaweza kupata uchovu na mabadiliko ya namna wanavyojisikia.
Wataalamu wa lishe wanashauri kutumia nafaka zisizokobolewa kwa kuwa zina nyuzinyuzi na virutubisho vingi. Mfumo wa ulaji unaojumuisha nafaka hizo ulihusishwa na maboresho ya afya ya kihisia katika utafiti wa mwaka 2017.
5. MTINDI
Mtindi usioongezewa sukari nyingi una bakteria rafiki wanaoweza kusaidia afya ya mfumo wa chakula. Wanasayansi wamekuwa wakichunguza uhusiano uliopo kati ya utumbo na ubongo, ambao unaonyesha namna mifumo hiyo miwili inavyoweza kuwasiliana na kuathiriana.
Tafiti mbalimbali zimeonyesha kuwa bakteria rafiki wanaopatikana kwenye vyakula vilivyochachushwa wanaweza kuwa na mchango katika afya ya mwili na akili. Hata hivyo, bado kuna haja ya kufanya tafiti zaidi kuthibitisha kiwango cha manufaa yake katika kuboresha hali ya kihisia.
JAMBO LA KUZINGATIA
Chakula bora kinaweza kusaidia afya ya kihisia, lakini si mbadala wa matibabu. Ikiwa huzuni, wasiwasi au mabadiliko ya hisia yanaendelea kwa muda mrefu na kuathiri maisha yako, ni muhimu kuzungumza na daktari au mtaalamu wa afya ya akili.